Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA yashiriki mahafali ya 41 kidato cha sita Sekondari ya Jangwani, elimu ya bima yatolewa; kuendeleza ushirikiano
25 Apr, 2025
TIRA yashiriki mahafali ya 41 kidato cha sita Sekondari ya Jangwani, elimu ya bima yatolewa; kuendeleza ushirikiano

Aprili 24, 2025

Katikati ya jiji la Dar es Salaam eneo la Jangwani karibu na soko maarufu la Kariakoo inapatikana moja kati ya shule kongwe Tanzania iliyoanzishwa Mei 28, 1928, Shule ya Sekondari ya wasichana Jangwani. Aprili 24, 2025 yamefanyika mahafali ya 41 ya kidato cha sita ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ilipata heshima ya kushiriki kama Mgeni Rasmi.

Akitoa hotuba yake Mgeni Rasmi, Meneja wa TIRA Kanda ya Mashariki Bw. Zakaria Muyengi kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware ameupongeza uongozi wa shule hiyo pamoja na wanafunzi kwa ufaulu mzuri katika mitihani ya kitaifa kwa miaka mbalimbali na kuahidi Mamlaka kuendeleza ushirikiano nao ambapo TIRA na wadau wa Bima watatoa msaada wa samani mbalimbali zikiwemo meza na viti kulingana na upungufu uliopo lakini pia itasaidia baadhi ya wanafunzi wenye changamoto za ulemavu kupata bima za afya na kusaidia ujenzi wa jengo la kulia chakula, ikiwa ni changamoto zilizoainishwa.

Aidha, Mamlaka ilitoa ujumbe kwa walimu, wazazi na wanafunzi kutumia bidhaa mbalimbali za bima ikiwemo bima ya maisha na bima za kawaida ili kuweza kujikinga na majanga yasiyotarajiwa, lakini pia walikaribishwa Ofisi za Mamlaka hiyo kupata semina zaidi kuhusu masuala ya bima.

Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi. Bhoke Nyagonde ameishukuru TIRA kwa ushirikiano walioonesha na msaada uliotolewa na kusisitiza lengo lao kubwa ni kuongeza uzalendo na kutoa elimu bora ili kujenga wasichana wazalendo kwa taifa lao na kuwa viongozi bora.

Moja ya mikakati ya Mamlaka ni kuhakikisha elimu ya bima inaanzia kwa watoto na vijana kama taifa la kesho na hivyo wakati wote hufanya semina na mikutano mbalimbali kwa wanafunzi na wanachuo ili kuhakikisha elimu ya bima inamfikia kila mmoja huku ikiendeleza ushirikiano katika kukuza sekta ya elimu nchini.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA