TIRA yawanoa Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Tabora

Tarehe 15 Septemba 2025 Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imefanya Mkutano na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Tabora (TABORA PRESS CLUB) kwa lengo la kutoa elimu kwa waandishi hao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya bima nchini na Mamlaka kwa ujumla hususan kuhusu majukumu ya Mamlaka, mchakato wa usajili wa watoa huduma za bima, namna ya kushughulikia malalamiko ya wateja na mifumo ya kidigitali inayotumika na Mamlaka hiyo katika kutekeleza majukumu yake.
Wakati wa Hotuba yake Bi. Awanje Matenda, Meneja wa Ofisi ya Mamlaka Kanda ya Magharibi ambako Semina hiyo iliendeshwa alisema, Mamlaka ina wajibu wa kusimamia, kudhibiti na kuendeleza sekta ya bima nchini Tanzania. Na Majukumu mengine ni pamoja na Kutoa leseni na kuhakikisha watoa huduma za bima wanazingatia sheria, kanuni na taratibu, Kutoa elimu ya bima kwa umma kuhusu umuhimu wa bima, Kulinda maslahi ya bima na walaji wake lakini pia Kuishauri Serikali kuhusiana na Masuala ya Bima. “Waandishi wa Habari ni Daraja kati ya TIRA, Wadau wa Bima na Wananchi, hivyo tunaomba mkandike vitu vya kweli na vya uhakika kuhusu masuala ya bima kwani hili ni suala mtambuka linalotakiwa kujulikana na jamii ili Majanga mengi yaweze kukingwa na kufidiwa” Alisisitiza Meneja Awanje.
Naye Afisa Bima Bi. Lea Mwakanosya kutoka Ofisi hiyo ya Kanda, alieleza namna ya kusajili aidha kampuni au wakala na huduma yoyote ile ya kutoa huduma za bima nchini na kueleza baadhi ya Vigezo na Masharti ya kufuata ambapo kikubwa zaidi lazima Mtoa huduma awe amesajiliwa rasmi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania. Baadhi ya vigezo vingine ni pamoja na kuwa na mtaji unaokidhi vigezo vya kisheria, Kuwa na miundombinu na rasilimali watu inayofaa, Kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpango wa biashara, taarifa za kifedha, na cheti cha usajili kutoka BRELA, Kupitia mchakato wa uchambuzi wa maombi na vibali kutolewa kwa waliokidhi masharti na kadhalika.
Mafunzo hayo yalihitimishwa na Bwn. Paul Nicholaus, Afisa TEHAMA wa Mamlaka hiyo alipoelimisha juu ya mifumo ya kidigitali inayoboresha utoaji huduma na usimamizi wa sekta ya bima kwa ujumla. Miongoni mwa Mifumo aliyoielezea Afisa huyo ni pamoja na Mfumo wa TIRA MIS (Management Information System), Mfumo wa usimamizi wa taarifa za bima unaowezesha kampuni kuwasilisha taarifa kwa njia ya mtandao na ndio unaowapa Polisi na Raia taarifa za uhai wa bima kwenye vyombo vya moto.
Si hivyo tu bali Afisa huyo alieleza Management System ambao ni Mfumo wa kushughulikia malalamiko kwa njia ya kidigitali na mwisho kabisa alieleza juu ya Online Licensing Portal ambao ni Mfumo wa usajili wa watoa huduma wa bima kwa njia ya mtandao.
Waandishi wa habari walipata nafasi ya kuuliza maswali na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya bima nchini, hasa maeneo ya uelewa mdogo wa wananchi na ucheleweshaji wa fidia. Mamlaka iliahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima na haki za walaji na kwamba mikutano ya aina hii itaendelea kufanyika mara kwa mara.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA.