Zanzibar na utayari mkubwa wa kuongeza matumizi ya bidhaa za bima
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inashiriki Maonesho ya 11 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar. Ikiwa ni muendelezo wa utoaji elimu ya bima lakini pia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuadhimisha Miaka 61 ya Mapinduzi.
Haya ni baadhi ya maoni ya wananchi kuhusu Maonesho hayo, “Nilikua napenda sana kufahamu kuhusu bima na faida zake, na leo hii kutembelea hapa TIRA kumenipa elimu ya kutosha nawashukuru sana wataalamu hawa walionipa elimu hii sasa nitazidi kuongeza matumizi yangu katika bidhaa za bima” anasema Hadhir Ramadhan mkazi wa Unguja.
Afisa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Oscar Mallya anasema “Maonesho haya yanawaleta pamoja wananchi mbalimbali ambao pia wanatamani kufahamu masharti na vigezo kabla ya kuwa mtoa huduma za bima lakini na sheria nyingine katika sekta hii, hivyo tunafahamisha na kuwapa elimu stahiki”
Ikiwa ni siku ya kumi na moja (11) tangu kuanza kwa maonesho hayo ya 11 ya Kitaifa ya Biashara Zanzibar, elimu kuhusu matumizi ya bima imeendelea kusisitizwa. Katika kuunga mkono Maadhimisho ya 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni TIRA na wadau wake walikabidhi mfano wa hundi ya milioni 321 kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
Maonesho haya yapo kwa siku kumi na tano katika viwanja vya Dimani Fumba, Unguja kama sehemu ya kuadhimisha miaka 61 ya Zanzibar na kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika 12 Januari 2025 Gombani Stadium, Pemba.
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA