Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha uliozinduliwa ni chachu kubwa katika kuikuza sekta ndogo ya bima nchini kwani utaweza kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha ikiwa ni pamoja na huduma ya bima kwa wale ambao hawajafikiwa na huduma hiyo.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Mussa Juma wakati wa uzinduzi wa mpango huo Jijini Dodoma na kuongeza kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini pamoja na watoa huduma za bima watajipanga kwa pamoja ili mipango yao iende sawa na mpango mkuu wa Serikali kwa miaka kumi ijayo kuanzia 2020 hadi 2030.

Dkt. Juma alieleza kuwa tayari Mamlaka imeshabainisha maeneo yanayopaswa kuboreshwa katika sekta ya bima ambayo ni kitaaluma na kiutafiti ili kuhakikisha Sekta ya Fedha inaendelea kuwa himilivu, yenye uweledi na yenye uwezo wa kushindana na mabadiliko mbalimbali katika sekta ya uhuma na fedha.

Pia, kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini, TIRA itahakikisha kampuni za bima zinatekeleza matakwa ya mpango huo ili kufikia malengo ya sekta ya fedha kuchangia zaidi katika maendeleo ya Taifa.  Kamishna wa Bima alisema pamoja na mpango huu kuchochea huduma za bima, utatumika pia kama nyenzo ya kutatua changamoto zilizopo kwa kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kulinda watumiaji wa huduma za fedha na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha.

Mpango huo ambao utekelezaji wake inatarajiwa kuchukua miaka kumi (2020-2030) umelenga: kukuza utoaji wa huduma za kifedha jumuishi, kuongeza kwa asilimia 10 bidhaa au huduma mpya katika soko la bima, asilimia 50 ya watu wazima nchini kuwa wamefikiwa na kuitumia huduma ya bima.

Pamoja na hayo, umelenga kupanua wigo wa njia za uuzaji na usambazaji wa huduma ya bima kwa gharama nafuu, kuuganisha mifumo ya TEHAMA katika sekta ya bima, kuongeza idadi ya kampuni zinazotoa huduma ya bima za kilimo na mifugo ili kuongeza idadi ya wakulima na wafugaji wanaotumia bima.

Kutokana na kutoa huduma kwa wananchi, pia mpango utahakikisha uwepo wa mfumo thabiti wa kushughulikia malalamiko ya watuamiaji wa huduma za kifedha pamoja na kampuni za bima kwa kuzingatia vigezo vya mitaji na ukwasi.

Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ulizinduliwa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.