Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo A. Saqware wakati wa mkutano na Maafisa wa Bima wa benki zinazotoa huduma ya bima kwa wateja yaani benki – wakala wa bima. Amewaambia maofisa hao kuwa nia ya Serikali ni kuona sekta ya bima inatengeneza faida kwa watu wanaowekeza kwenye biashara hiyo na hivyo kuvutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi.

Kamishna alifafanua kuwa ili kuweza kufikia lengo hilo wadau wa bima wana jukumu la kufanya kazi kwa weledi mkubwa, kufuata misingi na sheria iliyowekwa na Serikali pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa wa bima katika mabenki hasa eneo la uandikishaji wa bima.

Akielezea nia ya Mamlaka Dkt. Saqware alisema “tunapenda kuona soko linaloendeshwa kwa weledi, soko la bima ambalo linafanya kazi kwa faida na soko ambalo linapanuka na kuwafikia Wananchi walio wengi”  Alisisitiza kuwa soko likifanya kazi vizuri itakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Serikali wa Kukuza Sekta ya Fedha 2021 -2030.

TIRA imekutana na wawakilishi wa mabenki ili kujadili mwongozo kwa ajili ya uendeshaji wa huduma za bima kupitia mabenki hapa nchini. Mwongozo huu unatarajiwa kuanza mara baada ya majadiliano na wadau mbalimbali kukamilika ambapo watoa huduma katika mabenki watatakiwa kuufuata.