Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Jamal Kassim Ali ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) kuhakikisha kuwa sekta ya bima inatoa kinga kwa sekta muhimu za uzalishaji wa mali ghafi za viwandani.

Mh. Ali ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa sita wa baraza la pili la wafanyakazi la mapitio ya mapendekezo ya bajeti ya Mamlaka kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 lililofanyika Zanzibar.

“Mhe. Magufuli wakati akizindua Bunge la 12 na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi la 10, wote kwa pamoja waliweka mkazo katika maendeleo ya shughuli za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na kuvutia Uwekezaji kuwa sehemu muhimu katika ukuaji wa uchumi” alisema Mh. Ali.

Kwa dhana hiyo, kuna uhitaji mkubwa sana wa sekta hizo kukingwa na huduma za bima kwani itasaidia kuwalinda wananchi dhidi ya majanga yanayoweza kuwakumba na kuathiri jitihada zao za kujiimarisha kiuchumi.

Pia, Mh. Ali ameendelea kubainisha kuwa sehemu kubwa ya watanzania wanategemea kilimo na biashara ndogondogo, na ni mategemeo ya Serikali kuwa kufikia Mwaka 2030, asilimia 10 ya pato ghafi la soko la bima litatokana na kinga katika sekta ya kilimo ili kusaidia wananchi wengi wanapoteza mitaji na mazao yao kukingwa kikamilifu na sekta ya Bima.

“Ninakumbusha na nitaendelea kuwakumbusha, nguvu kubwa ielekezwe kwa wananchi wanyonge. Aidha, Menejimenti ya TIRA, Wafanyakazi pamoja na wadau mnatakiwa kuongeza kasi ya kutoa Elimu kwa Umma” alisisitiza Mh. Ali.

Akielezea mikakati ya Mamlaka Kamishna wa Bima Dkt. Mussa Juma amesema Mamlaka imeanza mchakato wa kuanzisha Kanzidata ya sekta ya bima ili kuiwezesha kupata taarifa muhimu zitakazosaidia katika kupanga mikakati na kurahisisha ufanyaji wa maamuzi katika kuendeleza soko la bima.