Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo Saqware amewataka Maafisa wanaoshughulikia fidia za bima kutoa huduma kwa uweledi ili wanufaika wa bima wapate haki zao kwa wakati. 

Dkt. Saqware aliyasema hayo wakati wa semina iliyohusisha wajumbe kutoka Umoja wa kampuni za Bima (ATI), Chama cha Madalali na Washauri wa Bima (TIBA) na maafisa madai wa kampuni za bima nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

Katika semina hiyo, mada kuhusu ulipaji wa fidia za bima zilijadiliwa kwa lengo la kuboresha huduma za bima nchini.

Amewataka maafisa hao kuwa na uweledi na uaminifu kwa wateja kwani Mamlaka iliwapa leseni za biashara ya bima inayowapa nafasi kukusanya ada za bima hivyo ni jukumu la kampuni kulipa fidia pale inapohitajika bila kumzungusha mteja.

Kamishna wa Bima amewataka maafisa hao kuwa makini na kutolipa  fidia kwa madai yasiyo halali akisistiza msimamo wa soko la bima nchini kuwa na weledi, pasipo uhalifu na kuhakikisha soko inatengeneza faida  kwa wawekezaji.

Aidha, ameyashauri makampuni ya bima kutoa mafunzo kwa maafisa madai ili wawe na uwezo wa kusimamia nafasi zao akiitaka kampuni kuwa na dawati la madai na mtu anayestahiki badala ya mteja kusikilizwa na mtu yeyote.

Wakati huo huo, Kamishna wa Bima amepokea ujumbe kutoka Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) ofisini kwake ambapo walipata nafasi ya kujadili mambo mbalimbali kuhusiana na maendeleo ya sekta bima.