Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini kutoa mafunzo na elimu ya bima kwa Jeshi la Polisi nchi.Kamanda Sirro ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la Mamlaka ya Bima nchini katika maonyesho ya Sabasaba.

"Ni muhimu kwa watumishi wote wa Jeshi la Polisi kupata mafunzo na elimu ya Bima ili kusaidia katika utekelezaji wa sheria ya bima nchini," alisema. Kamanda Sirro amesema Mamlaka ya Bima inawajibika kutoa elimu ya bima hata kabla wananchi hawajapatwa na majanga kwani kuna njia nyingi za kujikinga ama kupunguza athari za majanga hususan ajali za barabarani.

Dkt. Baghayo Saqware, Kamishna wa Bima nchini, ameeleza kuwa Mamlaka ina mipango mbalimbali ya kutoa elimu kwa Jeshi la Polisi na kupitia ofisi za kanda Mamlaka itaendelea kutoa elimu kwa watumishi wote wa Jeshi hilo.

"Wito na maelekezo yako tumeyapokea na tutatekeleza kwa njia inayoweza kuwa rahisi kwa pande zote mbili kwani lengo la serikali ni kuwalinda wananchi dhidi ya majanga," alisema Dkt. Saqware.