Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware ameshughulikia malalamiko na kupata suluhu ya ulipaji wa mafao ya bima kwa zaidi ya wanuifaka Mia Mbili na tatu, (203) ambao ni wakata Bima (Policyholders) na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).

Kamishna wa Bima alipokea malalamiko hayo tarehe 21 Septemba 2020 Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ikiilalamikia Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa kushindwa kulipa mafao kwa wanufaika wa mfuko kwa wakati na Kampuni ya Ushauri wa Bima ya Intertrade Express Limited kushindwa kutoa ushauri sahihi wa kibima na kwa uweledi kwa mujibu wa Sheria ya Bima na Miongozo yake.

Akiongea na waandishi wa habari leo, jijini Arusha, Dkt. Saqware ameliagiza Shirika la Taifa la Bima (NIC) kulipa wanufaika wote wa skimu ya Bima ya  wafanyakazi wa NCAA kwa mujibu wa mkataba na makubaliano ya pande zote yaliyofanyika tarehe 09 Juni 2022 kabla au ifikapo tarehe 1 Julai 2022.

“Ninawaagiza kampuni ya bima ya NIC kuboresha mfumo wa kutunza kumbukumbu, kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi waliosababisha kutokea kwa makossa haya na kutoa taarifa ya utekelezaji wa maagizo haya kila baada ya miezi mitatu kuanzia tarehe ya tangazo hili” aliongeza.

Sambamba na maagizo hayo, Dkt. Saqware amepiga faini Shirika la Bima la Taifa, Kampuni ya Ushauri wa Bima ya Intertrade Express Limited na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Bima SURA Na. 394, ninawapiga Shiriki la Bima la Taifa faini ya Shillingi za Tanzania Milioni Kumi na Tano (Tsh 15,000,000.00) kwa makosa matatu” alisema Dkt. Saqware.

Pia, katika malalamiko haya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) wamepigwa faini ya ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania Milioni Mia Mbili Sitini na Nne Laki Nne Thethini na Tisa Elfu Mia Moja na Tisini na Nane ( TSh.264,439,198/=) kwa kosa la kushindwa kuwasilisha michango iliyokatwa katika mishahara ya waajiriwa ndani ya siku thelathini kwa mujibu wa Sheria.

Kwa upande wa Kampuni ya Ushauri wa Bima ya Intertrade Express Limited, wamepewa adhabu ya jumla ya Shillingi ya Kitanzania Milioni Mia Moja Sitini na Tano (Tsh. 165,000,000.00) kwa mujibu wa kifungu cha 72(5), 161(1)(2), 166(1) kwa makosa ya yote matatu.