TAARIFA KWA VYOMBA VYA HABARI KUHUSU VIWANGO VINAVYOKUBALIKA KISHERIA VYA TOZO LA BIMA KWA AINA MBALIMBALI ZA BIMA ZA KAWAIDA.

 

Ndg Waandishi wa Habari.

Leo tarehe 16 Julai 2018, Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini inapenda kutoa taarifa kuhusu viwango mbalimbali vya tozo elekezi za bima katika biashara za bima za kawaida (yaani General Insurance).

Kwa mujibu wa kifungu namba 72(1) cha Sheria ya Bima Namba 10 ya Mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2017 Kamishna wa Bima Nchini amepewa Mamlaka ya kutangaza kupitia ya gazeti la serikali viwango elekezi vya tozo mbalimbali za Bima.

Ili kutekeleza matakwa ya Sheria Kamishna kupitia tangazo la Serikali No. 251 la tarehe 08/06/2018 ametangaza viwango vya tozo vinavyotakiwa kulipwa ili kupata huduma za madaraja mbalimbali ya bima za kawaida (General Insurance) kuanzia Julai 1, 2018 kama inavyoonekana katika tovuti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima (TIRA).  

 

Ndugu Waandishi wa Habari.

Mwaka 2014 Chama cha Makampuni ya Bima (ATI) kwa kushirikiana na Chama cha Washauri na Madalali wa Bima kilimwajiri Mshauri na Mtaalam wa Hesabu za Bima ili kutathmini na kushauri viwango elekezi vya bima za aina mbalimbali katika soko la bima Tanzania.

Ieleweke kuwa viwango hivi tunavyotangaza rasmi leo si vipya bali ni vile ambavyo vilikuwa vikitumika awali ila sasa vinapata msukumo wa kisheria na kimamlaka.

Kwani kutokana na ukaguzi na utafiti uliyofanywa na Mamlaka kwa makampuni ya bima yenye usajili imebainika kuwa tozo za bima zimekuwa zikitofautiana kutoka kampuni moja hadi nyingine. Pia, mara nyingi tozo hizo zinakuwa katika kiwango cha chini ya thamani ya mali inayokatiwa bima na viwango elekezi. Utaratibu huu umeleta athari katika soko la bima kwa kutokuwepo kwa mizania ya uwiano kati ya thamani ya vitu vilivyokingwa na tozo zilizokusanywa kwa ajili ya fidia iwapo kutatokea janga.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Mamlaka ina jukumu la kulinda watumiaji wa bima yaani wananchi na kuendeleza soko, imechukua hatua zifuatazo na kufikia uamzi huu.

  1. Upembuzi wa hali ya soko: Mamlaka ilifanya upembuzi kwa makini vigezo vinavyotumika na makampuni katika kukokotoa viwango vya tozo za bima ambavyo ni muhimu katika kupanga viwango vitakavyotumika.
  2. Ushirikishwaji wa wadau: Kwa sababu viwango hivi vitatumika katika soko la ndani, Chama cha Makampuni ya Bima nchini (ATI) walishirikishwa na kimsingi Mamlaka inayataka makampuni yafuate viwango hivyo kwa mujibu wa sheria.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Kufuatwa kwa viwango hivi elekezi kwa aina mbalimbali za tozo za bima za kawaida, soko la bima nchini litanufaika katika maeneo yafuatayo.

  1. Kupunguza uwezekano wa makampuni ya bima nchini kukosa mitaji; Hii itayawezesha makampuni ya bima nchini kujiendesha na kulipia fidia stahiki kwa wananchi kwa wakati kwani kwa kutumia viwango hivi kutakuwa na uwiano sahihi kati ya madai ya fidia na uwezo wa kampuni kulipa fidia.
  2. Pia itakuwa ni rahisi kwa makampuni yetu ya ndani kutawanya viashiria vya hatari (Risks). Msingi mizuri ya ukadiriaji wa tozo za bima ikifutwa kwa ufasaha inakuwa ni rahisi kwa makampuni ya bima ya ndani kukubalika na makampuni ya bima mtawanyo ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza na kuimarisha kinga dhidi ya majanga kwa wateja wa bima nchini.
  3. Kuimarisha huduma kwa wananchi wa Tanzania; Kuendelea kuwahudumia wananchi kwa weledi kwa kuwahakikishia bima ni nguzo muhimu katika kuwalinda dhidi ya majanga ya kiuchumi, kijamii na kiafya.  

Ndugu Waandishi wa Habari.

Mamlaka inawaasa watanzania kuendelea kutumia huduma za bima kwa kuzingatia mambo yafuatayo.

 

  1.  Kukata bima za vyombo vya moto na za aina nyingine kwa viwango halali vinavyotambulika kisheria ili kukinga mali zao.
  2. Kuendelea kutoa taarifa za ukiukwaji wa sheria ya Bima unaofanywa na kampuni yeyote tunayoisimamia au mtu yeyote anayehujumu biashara ya Bima.
  3. Kuleta malalamiko yao kuhusu huduma za bima kwa Mamlaka iwapo watahudumiwa chini ya kiwango na makampuni yetu.

 

Kwa makampuni ya Bima.

  1.  Kufuata viwango halali vya utozaji wa bima mbalimbali zinazohusiana na daraja la kawaida yaani (General Insurance).
  2.  Kulipa fidia halali za wananchi walio na kinga za bima baada ya kupatwa na majanga.

Naniwashukuru kwa kunisikiliza.

 

Dkt. Baghayo A. Saqware.

Kamishna wa Bima.