KAMISHNA WA BIMA TANZANIA AWAELEKEZA MAKAMPUNI YA BIMA KUWAHUDUMIA WAHANGA WA AJALI YA CITY BOY.

Kamishna wa Bima nchini, Dkt. Baghayo A. Saqware ameyataka makampuni ya bima yaliyotoa bima kwa gari la abiria la City Boy nambari T983DCE na gari la mizigo nambari T486ARB yaliyopata ajali tarehe 04/04/2018 wilayani Igunga mkoani Tabora kuwahudumia wahanga waliohusika katika ajali hiyo mapema iwezekanavyo mara tu taratibu za upembuzi wa madhara ukikamilika.

“Biashara ya bima duniani kote imeanzishwa ili kulinda na kukinga wananchi na mali zao dhidi ya majanga, hivyo ni wajibu wa Mamlaka kuwakumbusha na kushirikiana na makampuni iliyosajili kuhakikisha wananchi wanafidiwa dhidi ya majanga” alisema Dr. Saqware.

Mamlaka imefanya jitihada za kuhakiki kama magari yaliyohusika katika ajili hiyo yana bima halali na imekatwa kutoka kampuni gani amabzo Mamlaka imezisajili.

Kwa mujibu wa mfumo wa kuhakiki uhalali wa bima za vyombo vya moto nchini, TIRA-MIS uliotengenezwa na Mamlaka, unaopatikana katika simu za kazi anuai (Smartphone) magari hayo yamekingwa dhidi ya majanga na kampuni ya Mgen Tanzania Insurance Ltd kwa gari la abiria la City Boy nambari T983DCE na Kampuni ya Bima ya Taifa (NIC) kwa gari la mizigo nambari T486ARB.

Mamlaka imeshawasiliana na makampuni yote na kutoa maelekezo kwa kampuni hizo kuhakikisha bima inafanya wajibu wake wa kukinga majeruhi na kuwahudumia ili warejee katika afya zao na waendelee na kazi zao za kila siku.

Pamoja na hayo Dkt. Saqware ametoa pole kwa wananchi waliyokuwa katika ajili hiyo, amewaasa watanzania kuhakikisha kuwa wanapanda magari yenye bima kwa kuhakiki uhalali wake kupitia mifumo iliyowekwa na Mamlaka.

“Mamlaka imewapa uwezo wananchi kuamua juu ya usalama wa maisha yao kipindi wakiwa safirini kwa kuhakiki bima za vyombo vya moto wanavyovitumia; hivyo kurahisisha utoaji wa fidia majanga yanapotokea” alisema Dkt. Saqware.

Kwa upande wake Masuhuhishi wa migogoro ya bima nchini, Jaji Mstaafu Vincent Lyimo amewaasa wananchini wanaotumia vyombo vya usafiri wa umma kuhakikisha kuwa majina yao yanaandikwa katika orodha ya abiria walio katika basi husika (yaani passenger Manifest).

“Ulipwaji wa fidia za bima hutegema sana orodha ya majina ya abiria waliokuwa kwenye chombo husika kipindi kinapopata ajali hivyo ni wajibu wa vyombo vya usalama na abiria kwa ujumla” alisema Jaji Lyimo.