Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (TIRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) kufuatia marekebisho madogo ya Sheria ya Bima Na. 10 ya mwaka 2009 imeanzisha Tovuti ya kulipia bima kwa shehena zinazoingizwa nchini. Tovuti hiyo imeanza kutumika rasmi kuanzia Januari Mosi 2018 kwa mizigo yote inayoingizwa nchini kwa njia ya bandari, anga, reli na barabara.

 

Kamishna wa Bima Nchini Dr. Baghayo A. Saqware amewataka waagizaji, Mawakala wa Usafirishaji, Mawakala, Madalali na Makampuni ya Bima nchini kutumia Tovuti hii ili kuimarisha na kukuza biashara ya Bima nchini. "Mfumo huu tuliouanzisha utaleta faida kwa taifa na kwa mwananchi mmoja mmoja, kwani utahakikisha usalama wa bidhaa za wananchi zilizokingwa hivyo kuepusha upotevu wa raslimali za watanzania". Pia jitihada hizi zimelenga katika kukuza mitaji ya makampuni ya bima nchini.

Kwa wahusika wote watakao kiuka kutumia Tovuti hii watakuwa wamevunja sheria na hivyo hatau kali zitachukuliwa dhidi yao.

Mlamaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (TIRA) inahakikisha kuwa biashara ya bima nchini inafanyika kwa kufuata taratibu zenye kuleta manufaa kwa taifa na kwa wananchi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Hivyo, kwa kadri muda unavyokwenda Mamlaka itahakikisha taswira ya biashara ya bima nchini inakuwa nzuri na wananchi wanafurahia huduma za makampuni yanayosajiliwa na kusimamiwa na Mamlaka.