Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Ndg. Emmanuel Tutuba ametaka wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) kuendelea kusimamia soko la bima kwa uweledi ili kuchangia ukuaji wa shughuli za uchumi nchini.

"Pamoja na kuonekana kwa faida ndani ya miaka miwili iliyopita yaani Mwaka 2019 na 2020 bado ni muhimu sana sisi wafanyakazi wa Mamlaka ya Bima na Washauri wa Serikali tukajiuliza ni kwa jinsi gani tutaendelea kusimamia soko la bima na kufanya liwe na tija na mchango mkubwa katika pato la taifa" alisema Ndg. Tutuba.

 Pia, ametoa maelekezo kwa Menejimenti na wafanyakazi kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa tasnia ya bima inaongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa kama inavyoelekezwa kwenye Financial Sector Master Plan.

Naye Kamishna wa Bima, Dkt. Mussa Juma alisema katika kipindi cha mwaka wa biashra 2019 na 2020 sekta ya bima iliandikisha tozo ghafi za bima zenye jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 813.761 na 851.863 mtawalia. Kwa kuzingatia mwenendo wa biashara ya bima katika miaka mitano iliyopita yaani kuanzia Mwaka 2015 mpaka 2020, uwezo wa soko la bima nchini uliimarika zaidi na soko kupata faida katika mwaka wa biashara 2019 na 2020. 

Kuimarika huku kumechangiwa na kupungua kwa madai hususan yatokananyo na ajali za magari ambapo katika miaka hiyo miwili ajali hizo zilitumia tozo za bima kwa asilimia 45 ikilinganishwa na asilimia 54 katika miaka mitatu iliyopita.