Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA kuhakikisha haki za wateja wa bima zinalindwa kwa mujibu wa sheria ili kujenga imani kwa wateja hao.

Mhe. Mhagama ametoa rai hiyo mwishoni mwa juma wakati akifunga mafunzo kwa wataalamu wa bima kutoka mamlaka hiyo juu kufanya uchambuzi mbalimbali wa mikataba ya Bima Mtawanyo yaliyofanyika Unguja, Zanzibar.

Waziri alisema “Mamlaka ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha mnawakinga Wananchi na majanga mbalimbali yanayoweza kutokea ili kuwasaidia kurudisha katika hali waliyokuwa nayo”.  Akimtaka Kamishna wa Bima Nchini ahakikishe makampuni yasiyojali haki za wateja kuchukuliwa hatua.

Mh. Mhagama alimwelekeza Kamishna wa Bima nchi  kuwa mkali na kuendeleze jitihada za kutoa adhabu kwa kampuni zinazokiuka sheria ya bima hasa eneo la kuwanyima haki wananchi waliokata bima kwa mujibu wa sheria ya bima na mikataba”.

Aidha, Waziri Mhagama aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa Serikali imeiwekea malengo TIRA ya kukuza upatikanaji wa huduma za bima nchini ili wananchi wengi waweze kukingwa na majanga mbalimbali ya kiuchumi na kijamii yanayoweza kuwaathiri.

Alisema, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu aingie madarakani amedhamiria kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ikiwa ni pamoja na kuifungua nchi yetu kimataifa. Akaongeza kuwa, kwa kufanya hivyo Sekta ya Bima inanufaika kwa kuvutia Makampuni Makubwa ya Bima kutoka nje kuja kuwekeza nchini.

Alifafanua zaidi kuwa kuja kwa kampuni hizo kubwa za uwekezaji nchini zinavutia pia wawekezaji wengine wakubwa kuja kuwekeza nchini ambapo mitaji itakua, ajira zitapatikana na uchumi wa nchi yetu utakua. 

Aliitaka menejimenti ya Mamlaka hiyo kuongeza bidii katika kufanya kazi kwani mwaka ujao kuanzia mwezi June itapimwa kwa utendaji wake katika majukumu iliyopewa na serikali, Alisema “Ifikapo June 2023, TIRA itapimwa kuhusiana na ufanisi kwenye eneo la Bima Mtawanyo pamoja kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa bima nchini kwa kulinganisha na idadi ya sasa”.

Kufanikisha hili aliitaka Mamlaka kujiwekea malengo la kimkakati la kuhakikisha asilimia 99 ya Watanzania wanakuwa na uelewa kuhusiana na umuhimu wa bima.

Aidha, kwa upande wa mafunzo alisema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uwezo wandani wa wataalamu wetu kuweza kutambua kiasi gani cha fedha kinatakiwakubaki ndani ya nchi rentetion na kiasi gani kinaweza kupelekwa nje ya nchi externalization. Aliishauri TIRA kuweka utaratibu wa kuwa na mafunzo maalum kwa watumishi wake kuwa na uelewa mpana wa bima mtawanyo ndani na nje ya nchi.

Mafunzo hayo yaliyojilikita katika bima mtawanyo yaligusa zaidi maeneo ya uandikishaji (underwriting), ulipaji madai na usimamizi wa biashara ya bima mtawanyo.

Mhe. Mhagama alisema eneo la bima mtawanyo ni kipengele muhimu katika kuhakikisha biashara ya bima nchini inakuwa himilivu kwani itawezesha upatikanaji wa mitaji, kutawanya majanga mbalimbali, kutoa uwezo wa kitaaluma na kimtaji katika majanga anuai na kuongeza uwezo wa soko kukabiliana na majanga.

Aliipongeza Mamlaka kwa kutoa gawio kwa Serikali ambapo mwaka 2022 Sekta ya Bima nimeelezwa kuwa imechangia Shilingi Bilioni 2.4 kama gawio la Serikali. Akaeleza kuwa ni  matarajio yake kuwa Mamlaka ya Bima mtaendelea kuongeza wigo wa Sekta ya Bima nchini.  

Naye, Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Baghayo Saqware aliimshukuru Mhe. Mhagama kwa kutoa maelekezo ambayo yataininua sekta ya bima nchini. Dkt. Saqware alimwahidi Mhe. Waziri kuwa maelekezo yote yatafanyika kazi ili wakati wa kupimwa kwa ufanisi wa TIRA, huduma ya bima iatuwa imeongezeka na kuwafikia wananchi walio wengi.