Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na wadau imeanza kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa makundi mbalimbali ikiwa ni kiashiria cha kuelekea kuanza matumizi ya bima ya kiislaam nchini.

Mafunzo hayo yameendeshwa Jijini Dar es Salaam kwa Menejimenti ya Mamlaka na Jijini Zanzibar kwa watoa huduma za bima, wananzuoni wa Dini ya Kiislaam pamoja na Baraza la Maulamaa.

Waziri, Ofisi ya Rais - Fedha na Mipango Mhe. Jamal Kassim Ally alizinduliwa mafunzo hayo na katika Hoteli ya Oceanic View ambapo aliitaka Mamlaka ya Usmamizi wa Bima nchini (TIRA), kupitia sheria na kanuni zilizopo na kufanya juhudi za haraka za kuruhusu huduma ya bima ya kiislamu nchini kwani huduma ya bima ya kiislaam itachangia ukuaji wa sekta ya bima.

Aidha, Mhe. Ally aliendelea kuwakumbusha Mamlaka pamoja na wadau wa bima umuhimu wa kuwa na bima ya kiislaam kwa ajili ya watanzania wa kipato cha chini.

Alisema “niendelee kuwakumbusha kuwa sehemu kubwa ya watanzania wanategemea kilimo na biashara ndogondogo, ni mategemeo ya serikali kuwa kundi hili la wananchi litakingwa kikamilifu”. Akaongeza kuwa, Wananchi wengi wanapoteza mitaji na mazao yao katika maeneo, hivyo ni matarajio ya Serikali kuwa bidhaa hii (Bima ya kiislamu) pia itagusa maeneo hayo.

Awali, Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Juma Mussa alimweleza Waziri kuwa Bima ya Kiislam ‘Takaful’ ni bidhaa mpya katika soko la bima na Mamlaka imejipanga kuhakikisha huduma hii inapoanza iwe na utaratibu unaokubali kwa kufuata misingi ya kiislaam lakini pia taratibu za Serikali kama zinavyoelekeza.

Dkt. Juma akaeleza mikakati ya Mamlaka kuelekea kuanza mafunzo na hatimaye matumizi ya bima ya kiislaam kuchukua hatua kama: kuanza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma za bima, kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa watumishi wa Mamlaka ili wawe na ujuzi wa kuchambua bidhaa zinazotokana na aina hii ya bima, kimgine ni kuanza kazi ya kuandaa kanuni za bima ya Takaful (Takaful Insurance Regulations).

Alifafanua zaidi mikakati mingine ya TIRA kuwa ni pamoja na ushirikishaji wa wadau katika kutoa michango na maoni yao kuhusu huduma hiyo, kutoa elimu kwa Wananchi ili waweze kuitumia huduma hiyo baada ya taratibu kukaa sawa na kutoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari kuhusu bima hii ili twemde bega kwa bega wakati wa kuufahamisha umma kinachojiri kuhusiana na bima hiyo.

Mafunzo hayo yalifadhiliwa na Kampuni ya Bima ya First yaliudhuriwa pia na Kamishna wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja kutoka Wizara ya Fedha na Mipango - Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Menejimenti ya TIRA, watoa huduma za bima, wananzuoni wa Dini ya Kiislaam pamoja na Baraza la Maulamaa Jijini Zanzibar.

Maandalizi mbalimbali yanaendelea kufanyika kwa ajili kuleta bidhaa hiyo sokono chiniya uratibu wa TIRA kwa kushirikiana na wadau.