Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea pikipiki 26 kutoka sekta ya bima nchini kwa ajili ya Kikosi cha Usalama Barabarani.

Pikipiki hizo zenye thamani ya milioni 65 zimekabidhiwa na Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Mussa Juma kwa Mhe. Rais wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha hivi karibuni.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Jenarali wa Polisi Simon Siro alilitaka Jeshi la Polisi kutumia vitendea kazi hivyo kwa kazi zilizokusudiwa.

Awali akizungumza wakati wa tukio hilo, Dkt. Mussa alimwambia Mama Samia kuwa seka ya bima imefanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa jeshi la polisi nchini na kuwa ni wadau wakubwa wa sekta hiyo. Aliongeza kuwa wadau wa bima wamechangia kupatikana kwa vyombo hivyo ili kuwaongezea nguvu watendaji wa jeshi hilo.

Wadau wa bima waliochangia pikipiki hizo ni pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA), Kampuni ya Bima Mtawanyo Nchini (TANRE), Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Shirika la Bima la Taifa (NIC), makampuni ya bima ya Assemble, Mgen, Metro life na Tanzindia.