Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imesema itaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwa watoa huduma za bima nchini ili waweze kukua kibiashara na hivyo kuchangia pato la taifa.

Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Baghayo Saqware aliyasema hayo wakati wa mkutano na watoa huduma za bima mjini Unguja, Zanzibar uliolenga kijadili masuala mbalimbali yanayohusu kukuza soko la bima nchini.

Alisema "TIRA itaweka mazingira bora na wezeshi kwa watoa huduma za bima nchini ili waweze kuhudumia Wananchi ipasavyo"  na kuongeza kuwa "Mamlaka inatambua mchango wa watoa huduma za bima, hivyo iko tayari kushirikiana na makampuni ili kukuza biashara na uwezo wenu.

Aidha, Dkt. Saqware aliwakumbusha wadau juu ya vipaumbele vya Serikali katika kukuza sekta ya bima kuwa ni pamoja na kutekeleza mpango wa Serikali wa kuendeleza sekta ya fedha wa miaka kumi (10) wa 2020/2021 – 2029/2030.

Amewaeleza kuwa, katika mpango huu sekta ya bima inatakiwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za bima kutoka 14 asilimia hadi 50 asilimia ifikapo 2030, kwa upande wa uelewa iwe kutoka 30 asilimia ya sasa hadi 80 asilimia ifikapo mwaka huo.

Alifafanua zaidi kuwa, malengo hayo yatafikiwa kwa ushirikiano kati ya TIRA na wadau wa bima kwa ujumla. Kamishna alisema malengo yanaweza kufukiwa kwa kuongeza uwezo wa makampuni ya bima kifedha, kitaaluna na kuangalia suala zima la rasilimali watu katika shughuli za kuendesha biashara hizo.

Katika kukuza soko aliwashauri wadau kuwa wabunifu na kuongeza bidhaa za bima ambazo zinalenga uchumi wa bluu, kilimo, kuwatumia watu ambao hawako katika sekta rasmi kuuza bima. Jambo lingine likiwa ni kuifanya taswira ya sekta ya bima kuwa nzuri kwa watu tuaowahudumia hasa wateja wa bima, kwamba taswira ikiwa nzuri, huduma itaaminika.Akisisitiza suala la taswira, alisema, Mamlaka  haitakubali kamwe kuruhusu utoaji wa huduma mbaya katika soko ambayo itachafua taswira ya sekta nzima.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Said aliwataka watoa huduma za bima nchini kutoa huduma za bima zaidi ya magari ambazo wengi wao wanazifanya kwa asilimia kubwa. Alisema fursa ziko nyingi sana hasa wakati huu ambapo sera ya uchumi wa bluu umeshika kasi katika uchumi wa Zanzibar.

Bi. Khadija aliwata wadau pia kufanya kazi kwa uadilifu wakifuata sheria za nchi kwani wanaokiuka kufuata sheria katika utoaji wa huduma za bima, wanakwamisha maendeleo. Aliwaambia washiriki hao kuwafichua watu wanaotoa huduma za bima bila kufuata utaratibu ikiwemo wanaotoa bima bandia kwa wateja.

Mkutano huu ulikuja wakati wa ziara ya Kamishna wa bima kutembelea ofisi mbalimbali jijini Zanzibar ambapo alipata nafasi ya kumtembelea Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Bi. Salma Alli Hassan na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar ACP Zuberi Chembera.