Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (TIRA) leo imekutana na Chama cha Washauri na Madalali wa bima nchini (TIBA) ili kujadili masuala mbalimbali ya uendelezaji soko la bima na kutoa manufaa kwa wananchi wengi.

Akiongea katika mkutano huo Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Baghayo Saqware amesema uwepo wa Mamlaka katika kikao hicho ni kutokana na maombi ya TIBA kwa Mamlaka kuwasikiliza na kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayowakabili katika ufanyaji wa Biashara. Hivyo, Mamlaka iko tayari kujadili namna nzuri ya kuendeleza soko la bima nchini.

Pia, Kamishna aliwaomba wanachama wa TIBA kufanya majadiliano yao kwa kuzingatia vipaumbele vinne vya Mamlaka katika kuendeleza soko la bima ambavyo ni kuongeza na kukuza uwezo wa soko la bima (Kimtaji na Kitaaluma), kuimarisha taswira ya soko la bima nchini (Insurance Image), kuimarisha mifumo ya Tehama ili kurahisisha utoaji wa huduma za bima (Automations) na kupanua wigo wa utoaji wa huduma za bima nchini (Insurance penetration).