Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kutumia njia mbadala kumaliza mashauri ya bima nje ya Mahakama.

Mhe. Prof. Juma alisema ni wakati muafaka sasa kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho kwenye ya sheria ya bima kwa nia ya kuwezesha mashauri ya bima kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi kabla ya kupelekwa mahakamani.

Mhe. Prof. Juma ametoa ushauri huo mwishoni mwa juma hili ofisini kwake Jijini Dar es salaam alipotembelewa na ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Mamlaka hiyo ulioongozwa na  Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Baghayo Abdallah Saqware pamoja na Mwenyekiti wa wa Umoja wa Kampuni za Bima, Bw. Khamis Suleiman.  

“Huu ni wakati wenu wa kuangalia sheria zenu kwa sababu tangu mwaka 2020 sheria mpya ya usuluhishi imetungwa kwa lengo la kupunguza mashauri katika Mahakama hizi za kawaida’’ alishauri Prof. Juma.

Prof. Juma aliahidi kuwa mhimili anaouongoza utatoa ushirikiano mkubwa kwa Mamlaka katika kuhakikisha haki inatendeka. 

Akuwasilisha taarifa, Kamishina wa Bima nchini Dkt. Saqware changamoto inayotakiwa kutatuliwa haraka ni kuondoa udanganyifu na kupunguza ongezeko la kesi za madai kwani kuna kesi za madai 118 katika Mahakama mbalimbali nchini zenye thamani zaidi ya shillingi billioni 90.  

“kwa kutambua umuhimu wa Mahakama katika kuamua haki za watu, wakiwepo wadau wa bima, basi, Mamlaka  inaomba kesi za bima zipewe kipau mbele ili kusaidia kuwarudisha wadai katika hali zao kabla ya janga kama kanuni za bima zinavyoelekeza” alisema Dkt. Saqware.