Sekta ya bima nchini imeadhimisha siku ya bima kwa kufanya matembezi ya hisani kwa ajili ya kuchangia mahitaji kwa ajili ya shule tano zenye uhitaji maalum katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Matembezi hayo yaliyoandaliwa na ofisi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) kwa kushirikiana na makampuni ya bima yaliongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah ambapo yalianzia Minarani Kisonge – Michenzani - Madema - Maisara- Mnazi Mmoja  na kumalizikia katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil kwa ajili ya kuendesha harambee ya kuchangia  fedha kwa ajii ya shule hizo.

 Akiendesha harambee hiyo Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Abdallah alisema sekta ya bima ni muhimu katika ustawi wa jamii na uchumi wa taifa lolote duniani na kuongeza kuwa kitendo cha kuandaa matembezi ya hisani kutawasaidia sana vijana wenye uhitaji maalum katika shule ambazo zimelengwa.

Aliipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ofisi ya Zanzibar kwa jitihada ilizozifanya katika kufanikisha jambo hilo. Alisisitiza ushirikiano katika kufanikiwa kwa kila jambo “ni jukumu letu sote kuhakikisha tunashirikianakwa Pamoja katika kufikia malengo yaliyokusudiwa”

Aliongeza kuwa “kuwepo wa shughuli kama hizi katika sekta ya bima ni chachu ya maendeleo na kuisogeza karibu zaidi tasnia ya bima kwa wananchi”. Alisema anatambua kuwa matembezi hayo ni maalum kwa ajili ya kukusanya na kuchangisha kiasi cha fedha cha Shilingi 194 milioni ili kukidhi mahitaji ya vijana wenye uhitaji maalum katika shule tano (5) za Unguja ikiwemo Jann'gombe, Mwanakewerekwe "B” na  Kisiwandui kwa na kwa upande wa  Pemba ni Michakaeni  na Pandani. 

Awali Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija I. Said alimfahamisha Mhe. Abdallah kuwa

Sekta ya Bima nchini  kila Mwaka ina utaratibu wa kufanya shughuli mbalimbali za kuadhimisha siku ya bima yaani “Insurance Day”. Miongoni mwa shughuli hizo ni kuhakikisha kuwa jamii inanufaika na uwepo wa sekta hii kupitia kinga za majanga ya kiuchumi na kijamii. Alieleza Zaidi kuwa katika shughuli za kijamii, kwa mwaka huu Mamlaka kwa kushirikiana sekta ya Bima na baadhi ya mabenki nchini imeandaa matembezi ya hisani ili kupata fedha za kuweza kusaidia watoto wenye uhitaji maalumu katika shule tano zilizobainishwa kuwa na uhitaji wa vifaa mbalimbali katika eneo la Unguja na Pemba.

Alifafanua kuwa “uhitaji uliobainishwa katika shule hizo kama vifaa vya kusomea alama za nukta nundu, fimbo za kutembelea, gari kwa ajili ya kusafirisha walimu na wanafunzi, madawati ya watoto vyenye thamani ya shilingi 94 milioni. Hata hivyo, Naibu Kamishna wa Bima alimfahamisha Mhe. Mgeni Rasmi kuwa, TIRA kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya bima na baadhi ya wafanya biashara wameweza kukusanya fedha na vifaa venye thamani ya shilingi 38 milioni  ambazo zitatumika katika kununua baadhi ya mahitaji kwa watoto hao.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Ofisi ya Zanzibar iliendelea kuratibu zoezi la ukusanyaji wa michango hiyo na hatimaye kufikisha kiasi cha shilingi 191 milioni, kiasi ambacho kitakabidhiwa na Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, siku ya Ijumaa, tarehe 30 Julai 2021 katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil.