MAMLAKA YA BIMA TANZANIA YASISITIZA UBUNIFU.

Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima nchini (TIRA) imeyataka makampuni ya bima nchini kuwa wabunifu katika kutoa huduma za bima ili kuwafikia wananchi wengi hususan wanaoishi vijijini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa soko kutoka TIRA Bw. Elia Kajiba alipokuwa akifungua maonyesho ya pili ya bidhaa za bima nchini yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City.

“Ninawataka wafanyabiashara za bima kuwa wabunifu na waaminifu ili kuongeza imani ya wananchi katika bidhaa na huduma za bima tunazotoa” alisema Bw. Kajiba.

Katika maonyesho hayo mada mbalimbali zinajadiliwa ili kuhakikisha soko la bima nchini linanufaika na uwepo wa usimamizi madhubuti kutoka kwa Mamlaka ya bima na utoaji wa huduma nzuri na zenye hadhi kwa wananchi wa Tanzania.

Pia, Bw. Kajiba amesisitiza utayari wa Mamlaka kuhakikisha makampuni ya bima nchini yanaendelea kufanyakazi kwa kufuata sheria huku zikiendelea kukua kwa kufikia wananchi wengi hususan wananchi wanaoishi vijijini.

“Ni wazi kuwa lengo la serikali katika sekta ya bima ni kuwafikia angalau asilimia 50% watanzania watu wazima, lengo hili halitafanikiwa iwapo makampuni ya bima yaliyo na usajili nchini hayatashirikiana katika utoaji wa uhuduma za bima ikiwemo elimu kwa wananchi” alisema Bw. Kajiba.

Naye mwaandaji wa maonyesho haya Bw. Baraka Mtavangu ambaye ni Mwenyekiti wa Africa Digital Banking Summit Co Ltd amesema kuwa kutokana na wananchi wengi kutokuwa na elimu ya bima waliona ni vema wakaanzisha jukwaa hili.

“Mkutano huu wa siku mbili umelenga kuwafikia makundi mawili. Kundi la kwanza ni makampuni ya bima mbalimbali ambayo yatapata mada za kitaalama, pia wananchi watapata fursa ya kero zao kusikilizwa na kutatuliwa” alisema Bw. Mtavangu.

Mkutano huu utafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe Jumatano ya tarehe 28-29 Mei mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City.