Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware, ameyataka makampuni yote yanayofanya biashara ya bima nchini kutoa hudama zao kwa wananchi walio vijijini.

Hayo ameyasema wakati wa mkutano wa nusu mwaka uliowakutanisha wadau wa bima ili kujadili matokeo ya utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya serikali kuhusu sekta ya bima.

“Pamoja na kujadili namna ya kuwafikia 50% watanzania watu wazima ifikapo mwaka 2018, tumejadili utekelezeaji wa sheria hasa kwenye mabadiliko ya sheria ambayo yalitaka waagizaji na waingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kukatia bima bidhaa zao kupitia makampuni ya ndani” alisema Dkt. Saqware.

Sheria hiyo imeanza kutekelezwa mwaka huu na katika kipindi cha miezi mitatu ya Januari mpaka Machi makampuni ya ndani yameweza kutoa kinga kwa bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 209 ambazo zingepelekwa kwa kampuni za nje.

Aidha, alisema TIRA itaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau wa bima ili kuboresha sekta ya bima nchini kwani kazi ya serikali na taasisi zake ni kuweka mazingira wezeshi kwa biashara kufanyika” alisema.

Sekta ya bima imekua kwa asilimia saba kama uchumi wa nchi unavyokua na matarajio baada ya mkutano huo wataweza kuongeza ukuaji wa sekta kwa kuangalia maeneo ambayo yanahitaji maboresho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Sosthenes Kewe, alisema wananchi kununua huduma za bima bado ni changamoto, jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi.

Alisema kuna kazi kubwa ya kuwaelimisha wananchi ili wajue umuhimu wa kukata bima ili ziwasaidie wanapopatwa na majanga.