Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh. Queen Sendiga amewataka wananchi kuchangamkia fursa zilizoko katika sekta ya bima nchini. Hayo ameyasema alipotembelewa na Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware.

Katika majadiliano yake na Kamishna Mh. Sendiga alisema bima ni mkombozi wa mali za wananchini kwani ana uzoefu mzuri kutokana na fidia aliyopata baada ya kuunguliwa na nyumba yake.

“Mwaka 2014 niliunguliwa na nyumba yangu ambayo niliiwekea huko Dodoma, bahati nzuri ile nyumba ilikuwa na bima. Nililipwa fidia ya nyumba ile ndani ya muda mfupi baada ya kutoa taarifa kwa kampuni iliyonikatia bima” alisema Mh. Sendiga.

Pia, aliitaka Ofisi ya Kamishna kuendelea kutoa elimu kwa wananchini hususa ni wafanyabiashara ili waweze kukinga mali za dhidi ya majanga yanayoweza kuwakabili na msisitizo uwekwe kwenye shule, wamiliki wa mashine za viwandani na kilimo cha miti.

“Naamini Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini imejiwekea malengo ya kukuza upatikanaji wa huduma za bima nchini ili wananchi wengi waweze kukingwa na majanga mbalimbali ya kiuchumi na kijamii yanayoweza kuwaathiri, niko tayari kuunga mkono jitihada hizi” alisema Mh. Sendiga.

Kufutia jitihada hizo ameihakikishia Mamlaka kutoa ushirikiano katika kutoa elimu kwa umma kuhusu bima ili wananchi anaowangoza wapate fidia wanapopatwa na majanga.

Pia, kwa kushirikiana na uongozi wa Jeshi la Polisi katika wilaya zote atahakikisha vyombo vyote vya moto Mkoa wa Iringa vinanakingwa na bima.