Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kukuza sekta ndogo ya Bima.

Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha uliozinduliwa ni chachu kubwa katika kuikuza sekta ndogo ya bima nchini kwani utaweza kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha ikiwa ni pamoja na huduma ya bima kwa wale ambao hawajafikiwa na huduma hiyo.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Mussa Juma wakati wa uzinduzi wa mpango huo Jijini Dodoma na kuongeza kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini pamoja na watoa huduma za bima watajipanga kwa pamoja ili mipango yao iende sawa na mpango mkuu wa Serikali kwa miaka kumi ijayo kuanzia 2020 hadi 2030.

Dkt. Juma alieleza kuwa tayari Mamlaka imepokea maelekezo ya Serikali ambapo kupitia mpango huo  sekta ya bima inatakiwa kuboresha maeneo mbalimbali ya kitaaluma na kiutafiti ili kuhakikisha Sekta ya Fedha inaendelea kuwa juu, ya kisasa, yenye ushindani na kuweza kuhimili mabadiliko ya nyakati kwa wepesi na weledi mkubwa.

Ameongeza kuwa, kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini, TIRA itahakikisha makampuni ya bima yanautumia mpango huo ili kuleta tija na hivyo kuchangia vizuri katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.  Kamishna wa Bima alisema pamoja na mpango huu kuchochea huduma za bima, utatumika pia kama nyenzo ya kutatua changamoto zilizopo kwa kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kulinda watumiaji wa huduma za fedha na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha.

“Watoa huduma za bima walialikwa wakati wa uzinduzi wa mpango  huu  na kupata kujua nia ya Serikali katika kutoa huduma katika sekta ya fedha, hivyo ni imani yetu kuwa wataendelea kutoa huduma kwa kuzingatia dira ya mpango huo” alisisitiza Dkt. Juma. Wadau wa bima walishirikishwa kupitia vyama na umoja wao.

Hata hivyo, mambo muhimu yanayosisitizwa katika waraka huo na kutakiwa kutekelezwa mpaka kufikia mwaka 2030 ni pamoja na: kukuza utoaji wa huduma za kifedha jumuishi, kuongeza kwa asilimia 10 bidhaa au huduma mpya katika soko la bima, asilimia 50 ya watu wazima nchini kuwa wamefikiwa na kuitumia huduma ya bima.

Mpango huo pia, unaongelea kupanua wigo wa njia za uuzaji na usambazaji wa huduma ya bima kwa gharama nafuu kwa wananchi, kuuganisha mifumo ya TEHAMA ifikapo mwaka 2030 katika sekta ndogo ya bima, kuongeza idadi ya makampuni yanayotoa huduma ya bima za kilimo na mifugo na hivyo kuongeza idadi ya wakulima na wafugaji wanaotumia bima hizo. Mambo mengine ni kuhakikisha unakuwepo mfumo thabiti wa kushughulikia malalamiko ya watuamiaji wa huduma za kifedha pamoja na kampuni za bima kuzingatia vigezo vya mitaji na ukwasi.

Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ulizinduliwa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.