Hivi karibuni Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo Saqware amezindua miongozo mitatu ambayo itaanza Mei, 1 2022 katika kusimamia na kuwaongoza watoa huduma za bima nchini.

Miongozo iliyozinduliwa ni pamoja na Mwongozo ya Maafisa Wauza Bima (SFEs), Mwongozo wa Utoaji wa Huduma za Bima kwa Mtandao na Mwongozo wa Uendeshaji wa Bima ya Takaful. Miongozo yote inalenga kukuza soko pamoja na kupanua wigo wa utoaji wa huduma za bima, kuweka mazingiara wezeshi ya utoaji wa huduma hizo.

Wakati wa hafla ya uzinduzi Dkt. Saqware alielezea manufaa ya mwongozo wa Maafisa Wauza Bima yaani Sales Force Executives (SFEs) kuwa ni kuboresha wigo wa upatikanaji wa huduma za bima katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu hasa yale ambayo yana upungufu wa huduma hizo.

Kamishna wa Bima alisisitiza kuwa hii ni fursa ya kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu masomo ya bima. “Inakadiriwa takribani ajira 4,000 za moja kwa moja zitapatikana” Alieleza  Mkuu huyo. Hii maana yake ni kwamba vijana wachangamkie fursa zilizotajwa kupatikana katika sekta ya bima nchini.

Akifafanua zaidi Dkt. Saqware alisema miongozo ya maafisa wauza Bima itayagusa makundi makuu matatu ambayo ni Watu watakaoajiriwa kama Maafisa Wauza Bima, kwa upande mwingine ni  taasisi zilizosajiliwa na kupewa leseni na Mamlaka kutoa huduma za bima na watoaji wa huduma za bima zisizo za kitaasisi (rejareja) yaani  Non-corporate insurance services providers.

Katika kuandaa miongozo hii, Mamlaka imezingatia uhitaji wa huduma za bima kwa maeneo mbalimbali nchini ambayo hayajafikiwa kabisa ama yamefikiwa kwa uchache na huduma za bima. Hapa Kamishna wa Bima anaeleza wakati hafla ya uzinduzi kuwa “ili kuchagiza upatikanaji wa huduma za bima maeneo ambayo hayajafakiwa au yamefikiwa kwa uchache na watoa huduma za bima, Miongozo ya Maafisa Wauza Bima imeweka viwango vya chini vya uwepo wa Maafisa hao katika maeneo nje ya Dar es Salaam” ikiwa ni hatua ya kuhakikisha huduma zinafika huko pasipo na huduma ya bima.

Dkt. Saqware anaweka mpangilio na ufafanuzi vizuri jinsi ya kuwatumia maafisa wauza bima hao, anasema “madalali watakaopenda kuajiri Maafisa Wauza Bima watatakiwa kuajiri angalau Maafisa 20 ambapo asilimia 40 watawekwa mikoani’ Kwa mujibu wa miongozo akazitaka kampuni za Bima zitakazopenda kuajiri Maafisa hao zitatakiwa kuajiri angalau Maafisa 100 ambapo asilimia 50 watawekwa mikoani ili wafikie sehemu ambazo hazina huduma za bima.

Pia aliwaelekeza  Mawakala wa bima kwamba “watakaopenda kuajiri Maafisa Wauza Bima watatakiwa kuajiri angalau Maafisa 10 ambapo asilimia 30 watawekwa mikoani” Akizigeukia Benki-Wakala (Bancassurance agents) na kuzielea kuwa “wataajiri Maafisa Wauza Bima angalau Maafisa 100 ambapo asilimia 70 watawekwa mikoani”. Hii ndio dhana ya sekta ya bima kutengeza ajira kwa vijana.

Kiru kikubwa cha kuzingatia ni kwamba “hakuna Afisa Muuza Bima atakayeidhinishwa na Mamlaka kabla ya kusajiliwa na mtoa huduma husika”. Alihitimisha juu ya miongozo inayohusu Mafisa Muuza Bima.