SEKTA YA BIMA YA CHANGIA UJENZI WA VYOO VYA MFANO KWA WATOTO WA KIKE .

 

Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Baghayo Saqware hivi karibuni amekutana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasilisha mchango wa sekta ya Bima katika jitihada za kuunga mkono juhudi za kumwekea mazimgira mazuri mtoto wa kike awapo shuleni.

 

Katika shughuli hiyo, Dkt. Saqware aliambatana na maafisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima pamoja na mwakilishi wa kampuni za Bima Bi. Violet Mordechai na kuwasilisha kiasi cha milioni Thelathini na Tatu (Tsh. 33,000,000.00) ili kusaidia katika ujenzi wa choo cha mfano kwa ajili ya mtoto wa kike.

 

Dkt. Saqware amesema kuwa wameshirikiana na umoja wa kampuni za Bima ambao wametoa kiasi kwa ajili ya kujenga vyoo viwili ambapo Mamlaka imetoa gharama za ujenzi wa choo kimoja, hivyo kwa pamoja kama sekta ya Bima imetoa kiasi kwa ajili ya kujenga vyoo vitatu.

 

“Tunashukuru kwa wabunge kuwa na wazo hili, tutaendelea kushirikiana nao na sisi kama Mamlaka na sekta ya bima kwa ujumla tuko kuhakikisha kwamba tunaunga mkono juhudi zozote zile ambazo zinaondoa umasikini wa mtanzania au mwananchi wa kawaida, alisema Dkt. Saqware.

 

Naye Mh. Ndugai Spika wa Bunge amewashukuru sana Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima (TIRA) na sekta kwa ujumla kwa mchango huo na kuisema kuwa choo kitakachojengwa katika kila jimbo ni cha mfano kwa maana ya Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji ili waendelee kujenga vyoo vyenye hadhi hiyo ili kumhifadhi mtoto wa kike.

 

“Tunafahamu tatizo la vyoo katika shule zetu ni kubwa sana kwani watoto ni wengi na matundu ya vyoo ni machache, hivyo nitoe wito kwa wadau wengine nchini kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ili watoto wetu wajisitiri katika vyoo safi na salama, aliongeza Mh. Ndugai.

 

Kwa upande wake Bi. Magret Sitta, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake amesema “Tunawashukuru sana TIRA na sekta kwa ujumla kuwa nasi katika kuhakikisha mtoto wa kike anahifadhiwa katika choo chenye hadhi na cha mfano, huduma hii imelenga kuwafikia pia walemavu walio katika shule zetu”.

 

Pia, Kamishna aliwaomba viongozi hao waendelee kuwa chachu ya kuhamasisha elimu ya bima kwa wananchi ikiwemo za maisha, kilimo, majengo na afya katika mikutano yao na wananchi.