Sekta ya bima nchini imechangia shilingi milioni 100 kwa ajili ya Watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao yaani ‘Watoto Njiti’ wakati wa mbio za marathon za bima zilizofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam.

Akitoa salaam za shukrani kwa washiriki wa mbio hizo, Katibu Mkuu wa Wazira ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof.  Abel Makubi kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhesimiwa Dkt. Dorothy Gwajima alisema Serikali inawapongeza waadaaji wa mbio za marathoni zenye lengo la kuchangisha fedha kwani bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya watoto njiti.

Prof.  Makubi aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa mahitaji mengi bado nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa la vifo vya watoto wachanga chini ya mwezi mmoja ambapo lazima kuwe na jitihada za kupunguza vifo hivi. Alifafanua kuwa vifo hivi vinachangiwa kwa asilimia kubwa sana na watoto wanaozaliwa kabla ya muda, yaani wanaozaliwa kabla ya mimba kufikisha miezi 9.

“Takwimu zinaonyesha kuwa katika ya asilimia 13 -17 ya watoto wote wanaozaliwa Tanzania wanazaliwa njiti” alieleza Prof.  Makubi. Aliwaeleza wananchi waliofika katika tukio hilo kuwa watoto hao huitaji huduma maalum za uangalizi wa karibu ili waweze kukua vizuri na kwenda makwao wakiwa na afya iliyoimarika.

Serikali inafanya jitihada mbalimbali katika kuokoa watoto njiti ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afya kuratibu progamu mbalimbali ambazo lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano. “Programu hizo ni pamoja na kuanzisha wodi za matibabu za watoto wachanga na watoto waliozaliwa kabla ya muda (neonatal care units and Kangaroo Mother Care ward) kwenye hospitali za wilaya na manispaa, zoezi ambalo linasimamiwa kwa karibu na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Wizara ya Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na linaendelea kwenye mikoa kadhaa ya Tanzania, alifafanua Prof. Abel Makubi.   

Katibu Mkuu alipongeza jitihada zilizofanywa na wadau katika kukusanya fedha hizi kwa kusema “washiriki wa mbio hizi, mujisikie fahari kwa kuendelea kusaidia watoto wetu na watoto wa wenzetu kuendelea kupata huduma bora. Nawaomba muendelee kuwa na moyo huu wa kuchangia na msichoke kutoa misaada pale msaada unapohitajika”.  

Kwa upande wa Kamishna wa Bima Dkt. Mussa Juma alisema Mamlaka ya Usimamizi  wa Bima  Tanzania  ina  jukumu kubwa la  kuelimisha  wananchi  wa Tanzania kuhusu  huduma  za  Bima  ili  waweze  kuzitumia  katika kulinda  biashara,  afya, maisha  na  mali  zao. Hivyo   fursa kama hii   tunaiona ni muhimu  sana.

Alimfahamisha mgeni rasmi kuwa mkakati  unaofanyiwa  kazi  na  Serikali  kwa  sasa kupitia  Mamlaka  ni kuhakikisha  ifikapo   mwaka 2030  watanzania   asilimia  50   wawe  wanatumia  huduma za  bima  katika   nyanja  mbalimbali  kama  zilivyoainishwa katika  Mpango  wa Kuendeleza  Sekta  ya  Fedha 2020/2030.

Dkt. Juma alisema kilichotolewa kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ajili ya Watoto njiti ni mchango wa sekta ya bima kuhakikisha kuwa sekta hiyo unarudisha kwa jamii kwa kile wanachokipata na hivyo kuleta tabasamu kwa watoto hao.

Vile vile, Kamishna wa bima alieleza kuwa, shughuli kama  hii  haifanyiki  Tanzania  Bara  tu,  yatafanyika  matembezi  ya  hisani  ya  Bima  huko   Zanzibar    ili kuleta  hamasa  na  uelewa  kwa  Wananchi. Katika  tukio  hili, Rais  wa Zanzibar  na Mwenyekiti  kwa Baraza  Mapinduzi  Mheshimiwa Dkt Hussein Ally  Mwinyi  atakuwa  Mgeni  Rasmi. Pamoja  na  kutumia  njia  nyingine  na kuwafikia  Wananchi  mbio  za marathoni   na  matembezi  ya  hisani  ya bima yatakuwa  yanafanyika  kila  mwaka  kwenye  maeneo mbalimbali ya  Tanzania  Bara na  Visiwani. Tunaomba  Serikali  iendelee kutuunga  mkono   katika  juhudi  hizi.

Pamoja na kuzitaja changamoto zinazowakabili watotot wachanga Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili Prof. Lawrence Museru, aliishukuru sekta ya bima kwa kutoa msaada huo na kueleza kuwa “ni matumaini yangu kwamba kushirikiana kwetu kutaleta mabadiliko chanya katika kutoa huduma kwa watoto wachanga” akiongeza kuwa huduma kama hizi zikiendelea zitapunguza vifo vya watoto wachanga ili tuweze kufikia malengo ya mpango mkakati wa mwaka 2030 wa kuwa na vifo vya watoto wachanga chini ya vifo 12 kwa kila vifo 1000 vya watoto wachanga.

Hundi iliyokabidhiwa na Katibu Mkuu wa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Makubi kwa hospitali ya Muhimbili ni michango iliyotolewa na makampuni ya bima nchini kwa kuratibiwa na Umoja wa Makampuni ya Bima(ATI). Wadhamini wengine walioshiriki ni Doris Mollel Foundation na Vodacom.