Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutambua mchango wa makampuni ya bima katika kukuza uchumi wa nchi pamoja na kusaidia Wananchi wanapokutwa na majanga.

 

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipokutana na uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ulipotembelea ofisini kwake Vuga, Jijini Zanzibar ambapo Kamishna wa Bima Nchini Dkt Baghayo Saqware aliambatana na Naibu Kamishna Bi. Khadija Said na maafisa Mamlaka.

Mhe. Hemedi amesema Serikali inaridhishwa na muenendo ya makampuni ya bima katika kufidia jamii hasa wanapokutwa na majanga hatua ambayo inasaidia kupunguza athari zinazojitokeza wanapokumbwa na maafa.

Akiongelea masuala ya sheria na kanuni zinazoongoza soko la bima, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa mbali na uwepo wa sheria mbalimbali nchini bado wadau wa bima wanawajibika kuishauri Serikali kurekebisha sheria ili kuendana na mahitaji ya soko ikienda sambamba na kuboresha huduma za bima kwa Wananchi.

Vile vile, ameeleza kuwa bado jamii inahitaji elimu ya ziada kuhusiana na umuhimu wa kukata bima, hivyo ameutaka uongozi huo kuongeza juhudi za kuwafikia Wananchi hususan wawekezaji, wafanyabiashara na makundi yanayojishughulisha na biashara ili kujiunga na huduma hizo.

Akikabidhi miongozo ya bima Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo Abdallah Saqware amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa miongozo aliyomkabidhi imejumuisha mwongozo wa Maafisa Wauzaji wa Bima, Utoaji wa huduma za bima kidigitali, Bima ya Takaful na mwingine ukihusu Utekelezaji wa Viwango vya Kimataifa vya Taarifa za Kifedha kuhusu Mikataba ya Bima yaani IFRS 17.

Miongozo hii tayari imeanza kutoa fursa za ajira kwa vijana tangu ilipozinduliwa mnamo Aprili mwaka huu. Makampuni, watu binafsi wanaendelea kuwasilisha maombi kwenye Mamlaka.

Pamoja na hayo, Dkt. Saqware amueleza mkuu huyo kuwa Mamlaka inaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwekeza katika bima yenye kufuata misingi ya kiislam ya Takaful. Aidha, Kamishna alieleza kuwa ofisi yake inaendelea na kuhamasisha ukataji wa bima hususan maeneo ya kijamii ikiwemo masoko, majengo ya biashara, vivuko na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.