Taasisi za Serikali nchini zimeshauriwa kupata ushauri wa kitaalam kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kabla ya kukata bima katika iradi ake ili serikalii iweze kupata huduma stahiki kulingana na mahitaji yake.

Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo Saqware ametoa ushauri huo wakati akitoa wasilisho kwa washiriki wa mkutano mkuu wa wataalam wa ununuzi wa umma nchini sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Ununuzi wa Umma katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.

 Dkt. Saqware amewaambia washiriki zaidi ya 1,000 kuwa ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza kuhusiana na huduma za bima ni bora taasisi za umma zitakazohitaji huduma hizo zifike Mamlaka ili kupata ushauri wa kitaalam.

Katika wasilisho lake Kamishna wa Bima alipata nafasi ya kuelezea Sheria ya Bima Na. 10 ya Mwaka 2009 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2017 kifungu namba 133 kinachohusisha michakato ya ununuzi unaohusisha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ambapo bima kwa ajili ya bidhaa hizo zinatakiwa kukatwa hapa nchini badala ya kulipa sehemu ya bima nje ya nchini.

Kamishna alisema, wananchi na taasisi binafsi zimekuwa zikitumia sheria hii tangu ilipopitishwa na imesaidia sana kuondoa sintofahamu pale linapotokea tatizo kwani aliyemkatia bima mteja anakuwa nchi za nje.  Sheria hii imefanikisha waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kudai fidia zao kutoka kwa makampuni ya bima yanayofanya shughuli zake hapa nchini.

Mkutano huu uliozinduliwa na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa umeandaliwa na PPRA, PSPTB, GIPSA na PPAA. Mamlaka ni moja yataasisi za umma zilizodhamini mkutano huo na kupata tuzo ya udhamini na ushiriki.