Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) imetoa adhabu kwa kampuni nne za bima nchini kutokana na kuwa na mwenendo usiofaa katika utoaji wa huduma za bima nchini.

Kampuni hizi zimepigwa faini kutokana na kwenda kinyume na matakwa ya Sheria ya Bima Namba 10 ya Mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2017 kunakopelekea kampuni hizo kutotoa huduma stahiki kwa wateja wake.  

Akiongea jana katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Ofisi ndogo ya Dar es Salaam, Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Baghayo Abdallah Saqware alisema “Mamlaka imebainisha pasipo na shaka kuwa kampuni za bima za Insurance Group of Tanzania (IGT), Jubilee General Insurance, Resolution Insurance na UAP Insurance ndizo zilizohusika katika kadhia hii. 

Kwa upande wa Kampuni ya Insurance Group of Tanzania (IGT), alieleza kuwa imekuwa na matatizo ya kulalamikiwa kwa kutolipa fidia kwa wakati kwa mnufaika wa bima, ucheleweshaji wa mchakato wa madai pamoja kukataa madai bila kufuata misingi ya kibima pia kutolipa madai baada ya kutoa Hati ya Kukubali Madai yaani Discharde Voucher. 

Kamishna Dkt. Saqware alifafanua zaidi kuwa kampuni hii pia imeshindwa kutekeleza maamuzi ya Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) pamoja na kuchelewa kutoa idhini na malipo ya matengezo ya magari ya wateja wa bima wanaodai fidia.

Kufuatia mapungufu hayo, kwa mujibu kifungu namba 166(1 & 2) cha Sheria ya Bima nchini Kamishna wa Bima amechukua hatua dhidi ya Mwenyekiti wa Bodi, Afisa Mtendaji Mkuu, Afisa Fedha Mkuu na Meneja madai wa kampuni ndani ya IGT.

Akazitaja faini hizo kwa kampuni ya IGT: Mamlaka inatoa faini ya kiasi cha Tsh 5,000,000.00 kwa Mwenyekiti wa Bodi ya IGT kwa kutoishauri na kutosimamia vyema Menejimenti ya kampuni, hivyo kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao.

Pili, TIRA inatoa faini ya kiasi cha Tsh 5,000,000.00 kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa IGT kwa kutosimamia vyema utendaji wa kila siku kampuni hivyo kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao. Naye  Afisa Fedha Mkuu akapigwa faini ya kiasi cha Tsh Tsh 5,000,000.00 kwa kutoheshimu sheria ya Bima na kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao.

Huku Meneja wa Mdai na Fidia wa IGT faini ya kiasi cha Tsh 5,000,000.00 kwa kutoheshimu na kuzingatia sheria ya Bima na kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao. Dkt. Saqware akachukua nafasi hiyo kuiagiza kampuni ya IGT kulipa wadia wote 48 ambao imeshawapatia hati ya kukubali madai (Discharge Voucher) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya tangazo 10 Mei 2022.

Aidha, Kampuni ya Jubilee, Mamlaka imekuwa ikipokea malalamiko dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hii kuhusu mwenendo usiyofaa wa utendaji katika sekta ya bima hususan katika maswala yanayohusiana na madai.

Baadhi ya malalamiko ni kushindwa kutimiza mikataba iliyowekeana wateja wake amabo ni taasisi za serikali na binafsi ikiwemo Wizara ya Maji dhidi ya kampuni hiyo kutokubali kulipa malipo ya fidia kutokana na Kampuni ya ukandarasi ya Spencon kushindwa kutimiza wajibu wake wa kimkataba wa ujenzi wa miradi ya maji. Nyingine ni mradi wa maji Mamlaka ya Maji ya Mji wa Kigoma ambao ulikuwa umepewa kinga na Kampuni ya Bima ya Jubilee.

Kwa kuzingatia Sheria na taratibu za uendeshaji wa Biashara za Bima nchini, Mamlaka inachukua hatua nne kama zifuatazo: Kuiagiza Kampuni ya Jubilee kulipa kiasi chote cha Euro 511,065.49 kwa Wizara ya Maji kama ilivyoagizwa katika kikao cha tarehe 18. Novemba 2021 ndani ya siku 14 kuanzia siku ya tangazo hili tarehe 10 Mei 2022.

Hivyo, TIRA imetoa adhabu faini ya kiasi cha Tsh 10,000,000.00 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hii kwa kutofuata taratibu za kibima hivyo kuchafua taswira ya soko la bima kwa makosa wawili tofauti ambapo kila kosa litakuwa Tsh. 5,000,000.00.

Mwananchi Innocent Masinde alilalamikia utendaji mbovu wa Mtendaji Mkuu wa kampuni hii Ndg. Dipanka Achary na Mwanasheria Ndg, David Shoo kwa kutolipa madai yake kinyume na msingi wa uchakataji wa madai kama inavyotakiwa na taratibu na Sheria ya Bima Na. 10 ya Mwaka 2009.

Kwa upande wa Kampuni ya Bima ya Resolution. Mamlaka kwa  nyakati tofauti imekuwa ikikagua na kushauri namna nzuri ya uendeshaji wa kampuni hii baada ya kuona uwezo wake wa kifedha unazorota kutokana na usimamizi mbovu, mwenendo usiyo wa kitaalamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za ufanyaji wa biashara ya bima uliyofanywa na Wakurugenzi na Afisa Mkuu wa kampuni hii.

Kufuatia hayo, Msimamizi wa soko la bima ametoa adhabu ya kiasi cha Tsh 5,000,000.00 kwa Wakurugenzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hii kwa kila kosa la kutofuata taratibu za kibima hivyo kuchafua taswira ya soko la bima.

Mamlaka pia imetoa siku tisini (90) kuanzia 10 Mei 2022, kama ilivyoombwa na wawakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi katika kikao na Kamishna kilichofanyika siku ya Jumatatu tarehe 25 Aprili 2022, kukamilisha taratibu za kuweka mtaji kwa mujibu wa sheria.

Tena, Mamlaka inaweka zuio la kampuni hii kutoendelea kuandikisha na kuchukua Biashara yeyote mpya ama kufanya matangazo yeyote yanayolenga kupata biashara mpya mpaka pale watakapokamilisha takwa la kimtaji.

Hivyo, Watanzania na jumuiya ya wanabima wanajulishwa kuwa kampuni ya bima ya Resolution na wawakilishi au washirika wake wote HAWARUHUSIWI kufanya shughuli za biashara ya bima kuanzia Jumanne ya leo tarehe 10 Mei, 2022.

Mamlaka imeitaka Kampuni ya bima ya Resolution kuendelea kulipa madai yote yaliyopo na yatakayowasilishwa kwao kwa mujibu wa sheria. Wakati huo huo, Mamlaka itaendelea kufanya Uangalizi Maalumu wa Kampuni ya Resolution Insurance Company (T) Limited kwa lengo la ufuatiliaji wa karibu mwenendo na utekelezaji wa maagizo na ombi lao ya kurekebisha hali hiyo.

Hatimaye Kampuni ya Bima ya UAP. Kwa nyakati tofauti Kamishna wa Bima amekuwa akipokea malalamiko dhidi ya kampuni hii. Pamoja na Mamlaka kuelekeza kampuni hii kufanyia kazi na kutoa fidia kwa madai hayo kampuni hii imekuwa na tabia ya kutoshughulikia kwa haraka baadhi ya malalamiko ya wateja. Pia, kuchelewesha kwa malipo ya bima ya mteja ambapo Mamlaka inaigiza kampuni hii kulipa fidia mara ndani ya siku 7 kuanzia tarehe 10 Mei 2022.

Kamishna wa Bima alisema ”kutokana na Mamlaka kuwa na jukumu la kulinda watumiaji wa bima yaani wananchi na kuendeleza soko, inatoa onyo kwa kampuni za bima nchini zitakazochelewesha ama kuchezea haki ya fidia ya mwananchi”.

Kamishna amesema pia ”tunawaasa watanzania kuendelea kutumia huduma za bima nchini na kutosita kuleta Malalamiko yao kwa Kamishna wa Bima pindi wanapoona kampuni za bima haziwatendei haki”.