Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imezindua kituo cha ukaguzi wa bima za vyombo vya moto katika bandari ya Dar es Salaam, geti namba mbili ikiwa ni hatua ya kudhibiti mianya ya udanganyifu na utapeli unaoweza kufanywa na watu wasio waaminifu katika kutoa huduma za bima.

Hatua hii inalenga kuanza na magari yanayoshushwa katika bandari hiyo kutoka nje ya nchi ambayo yanapita Tanzania kwenda nchi nyingine, maarufu kama IT. Hatua itakayofuata ni ukaguzi wa magari yote bila kujali kama yanabaki nchini au yanaenda nje ya nchi.

Akizindua kituo hicho Kamishna wa Bima Dkt. Mussa C. Juma alisema kituo hicho kitakuwa kinatumika kukagua bima za vyombo vya moto kabla ya kutoka nje ya gate lolote na akifafanua zaidi kuwa “hii inamaanisha kwamba bima ya chombo husika itakatwa gari likiwa ndani ya bandari”. Dkt. Juma aliongeza kuwa ni jukumu la Mamlaka kufanya usimamizi, lakini pia kuhakikisha wateja wanalindwa na wanapewa bima sahihi zinazotambuliwa na mifumo ya TEHAMA ya Mamlaka.

Mkuu huyo akachukua nafasi hiyo kusisitiza kuwa “ni kosa la kisheria kwa chombo cha moto kutembea bila bima katika ardhi ya Tanzania, na hii haina mbadala ni muhimu kufuata matakwa ya kisheria”.

Aidha aliwataka wananchi kuwa huru kuchagua wapi watapata huduma za bima bila kupangiwa na mtoa huduma yeyote wapi akate bima. Alisema soko la bima ni huru na huria. “nifafanue na kuusisitiza umma, watoa huduma za bima na wadau wengine kwamba, soko la bima ni huru na huria hivyo mmiliki wa chombo cha moto yuko huru kukata bima ya chombo chake kwa kampuni ya bima, dalali wa bima au wakala wa bima yeyote kupitia mfumo mpya wa TIRA MIS,”  alisisitiza Dkt. Juma.

Utratibu huu umefanyika baada ya TIRA kupata kibali kutoka kwa Mamlaka ya bandari Tanzania (TPA) cha kuendesha shughuli hizo ndani ya bandari ya Dar es Salaam. Naye Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Elihuruma Lema alisema uzinduzi wa kituo hicho utaleta chachu na kuongeza ufanisi na kuongeza shehena ya magari yaendayo nchi Jirani kupitia bandari hiyo kwani watakuwa na uhakika wa bima waliyokata kabla ya kutoka nje ya geti.

Tukio hili liliudhuriwa na viongozi kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),  Kikosi cha Usalama Barabarani, Umoja wa Makampuni ya Bima Tanzania (ATI) na Umoja wa Watoa huduma za Forodha Tanzania (TFFA).