Viongozi wa Mamlaka ya Bima leo wamefanya makabidhiano ya Ofisi kufuatia uteuzi wa Dr. Baghayo A. Saqware kuwa Kamishna aliyoufanya Mh. Samia Hassan Suluhuh – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima zilizo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati akikabidhi ofisi, Kamishna aliyemaliza muda wake Dkt. Mussa C. Juma amewaasa watumishi kuendelea kumpa ushirikiano Kamishna mpya ili kuendeleza soko la bima na kutoa mchango stahiki katika uchumi wa taifa.

“Ninawaomba muendelee kutoa ushirikiano kwa kiongozi mpya kama mlivyokuwa mkifanya kwangu, tuendelee kushauri kwa uweledi bila kuweka maslahi binafsi kwa kila shughuli tunayoifanya” alisema Dkt. Mussa.

Pamoja na hilo, Dkt. Mussa alimuasa Dkt. Saqware kuendeleza program nzuri alizoziacha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha soko la bima nchini linaendesha kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ili kuboresha utendaji wa soko.

“Tumetengeneza mifumo ya kudhibiti biashara ya bima, pia mazoezi ya utoaji uelewa wa bima kwa wananchi ni vema yakapewa kipaumbele. Vilevile, ukaguzi wa watoa huduma za bima ni muhimu kuendelea kwani kumekuwa na mivutano kati ya wadau sokoni” alisema Dkt. Mussa.

Naye Kamishna wa Bima Dkt. Saqware alikiri kupkea taarifa ya makabidhiano kutoka kwa Dkt. Mussa na kuahidi kuendeleza pale alipoachia ili kukuza soko la bima kwa maslahi ya taifa.

“Ieleweke kuwa lengo letu ni moja. Kuendeleza tasnia ya Bima nchini. Tunaweza kuwa na mitazamo tofauti kiutendaji na kiutekelezaji lakini bado naamini tunawajibu wa kuleta tija katika soko la bima” alisema Dkt. Saqware.

Ningependa watumishi wa Mamlaka kuwa na ueledi katika kutekeleza majukumu yao, na pia kuhakikisha tunaowahudumia wanafurahia kufanyabiashara katika soko letu ili kuweza kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta yetu ya bima.

“Niwahakikishie wadau wote wa soko la bima nchini kuwa tutashirikiana, tutashauriana na kuja na namna bora ya kukuza soko letu na kuongeza mchango wa sekta hii katika pato la taifa” aliongeza Dkt. Saqware.