Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), kuzielekeza kampuni za bima nchini kuandaa ikataba ya bima kwa lugha ya Kiswahili ili kurahisisha uelewa na kutoa haki kwa wateja.

Mhe. Ulega amesema wananchi wengi wanaingia katika mikataba mbalimbali ya Bima ambayo inaandikwa kwa lugha ya kiingereza na matokeo yake wengi wamekuwa wakidhulumiwa haki zao kutokana na kutoielewa kwano imeandikwa katika lugha isiyoeleweka kwao.

Waziri Ulega aliyasema hayo alipotembelea Ofisi Ndogo ya Mamlaka hiyo iliyopo Jijini Dar es salaam kwa lengo la kusisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye mikataba na nyaraka mbalimbali zinazotolewa na taasisi za bima wakati wa kuhudumia wananchi.

Akiongeza kuwa kwenye huduma za bima kuna nyaraka nyingi ambazo zinatakiwa zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili kama vile mikataba ya bima (insurance policies), mkataba wa muda(cover note), fomu ya maombi (proposal form) na nyinginezo. Mhe. Ulega akaagiza “makampuni yanayofanya shughuli za bima moja kwa moja kwa wananchi sasa wanatakiwa kutafsiri mikataba yao iwe kwa lugha ya Kiswahili,”

Mkuu huyo alisema,  ili kuondokana na migogoro ya kibima baina ya Wananchi na Makampuni ya bima ni muhimu kuangalia upya lugha zinazotumika kwenye mikataba hiyo. Kuenenda na hili Waziri ameelekeza kuwa nyaraka zote zitatakiwa kutafsiriwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili ziweze kudhibitishwa na hatimaye kupewa Cheti cha Ithibati.

Wakati wa ziara hiyo, alijionea nyaraka mbalimbali ambazo tayari TIRA ilishazifanyia kazi baada ya kutoa maelekezo mwaka jana kuanza kubadili nyaraka wanazozitumia kuhudumia wateja kuwa katika lugha ya Kiswahili. Aliipongeza Mamlaka kwa kutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika kuhudumia Wananchi. “Namshukuru sana Kamishna wa Bima, amenihakikishia kwamba zile Bima zinazokwenda moja kwa moja kwa Wananchi ni lazima ziwe za lugha ya Kiswahili, lengo ni kuhakikisha Wananchi wengi wanakata Bima, na wanakwenda katika kukuza uchumi wa Taifa letu”. Aliongeza kuwa,  “sasa watakwenda kutumia lugha ya kiswahili kwa sababu ndio lugha inayoeleweka zaidi na ninayo imani kwamba wananchi wengi wataingia kwenye utaratibu huu wa bima kwa sababu kile kitu wanachokiingia watakuwa wanakielewa kwa urahisi”

Kwa upande wake Kamishna wa Bima kutoka katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania- TIRA Dkt. Mussa Juma amesema zoezi hilo linatarajiwa limeanza kufanyiwa kazi kwa kuziagiza taasisi zinazotoa bima nchini kutafsiri mikataba yao kwa lugha ya Kiswahili kwenye mikataba yao ambapo kufikia mwezi Juni zoezi hilo kuwa limekamilika.

“Wazo la kutafsiri lugha ya Kiswahili lilitokana na changamoto, maoni na malalamiko ya wananchi, wengi wanashindwa kulipwa haki zao kwa sababu wanakuwa hawajaelewa kilichoandikwa kwenye huo mkataba” alisema Dkt Juma na kufafanua kuwa, “mtu anakuwa na huo mkataba bila kuelewa kwamba analipwa au halipwi, na anapokuja kudai anaambiwa mbona tumeandika kwenye mkabata wako kwamba hiki kitu hakilipwi?, ndio maana tukaona kuna kila sababu ya kutafsiri mikataba hiyo ili kutowanyima haki wananchi”.

Itakumbukwa kuwa, serikali imekuwa ikitilia mkazo wa matumizi ya lugha ya kiswahili katika kazi mbalimbali za kuwahudumia Wananchi ili kuwepo na uelewa wa pamoja kwa kila mtu anachohudumiwa.