Wadau wa bima nchini hivi karibuni wamefanya mkutano kwa ajili ya kijadili viwango pendekezwa vya ulipaji wa fidia za kibima kwa wahanga wa ajali kwa kuzingatia bima ndogo (third party).

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ili kuwafahamisha wadau juu ya hatua hiyo lakini pia kupata maoni yao ili yafanyiwe kazi na hatimaye kuwa na waraka utakawaongoza watoa huduma za buma kufuata pindi wanapolipa fidia kwa wahanga hao.

Akifungua kikao hicho Kamishna wa Bima Dkt. Mussa Juma aliwaambia wadau kuwa umefika wakati wa kuondoa sintofahamu wakati wa kulipa fidia kwa watu ambao wamepata ajali kwani makampuni ya bima hayana viwango maalum vya fidia hizo. Aliwataka wadau kutoa mawazo na michango mbalimbali kwa ajili ya kuboresha waraka huo ambao utaanza kutumika mara tu ukikamilika. 

Mkakati huu umekuja baada ya TIRA kufanya utafiti wa kina na kugundua kwamba kuna tatizo la viwango vya  ulipaji wa fidia kwa wahanga wa ajali zinazohusisha vyombo vya moto. Kila kampuni imekuwa ikilipa fidia kwa viwango ambavyo imeviweka  yenyewe au kukubaliana na mhanga wa ajali.

Kufuatia hali hiyo,  Kamati inayoratibu zoezi hili ilichukua maoni ya wadau wote ambayo yanafanyiwa kazi kwa sasa na baadae yatarudishwa kwa wadau ikiwa ni hatua ya mwisho kabla ya kuwasilishwa serikalini.

Malipo ya fidia kwa wahanga wa majeraha na vifo hulipwa kwa kuzingazita vigezo mbalimbali kwa mfano; mtu aliyepoteza maisha kwenye ajali huangaliwa umri wake, kipato chake kutokana na kazi (kama ni mwajiriwa au amejiajri) Pamoja na shughuli za biashara anazozifanya. Kwa upande wa majeraha ya mtu, hutegemea ripoti na vipimo vya daktari vinavyoeleza mhanga huyo amepoteza uwezo wa kufanya kazi pamoja kiungo/viungo vya mwili kwa asilimia ngapi.

Utaratibu huu unaofanyiwa kazi na Mamlaka utaweka viwango sawa vitakavyotumika kilipa fidia na hivyo kuondoa mkanganyiko uliopo sasa.