Ongezeni utoaji Elimu ya Bima kwa Wananchi: Waziri Mkuu Majaliwa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa amezitaka taasisi zinazotoa huduma za bima kutoa huduma kwa Wananchi ili kuongeza wigo wa uelewa.

Mkuu huyo amesema hayo hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa mbio za marathoni za bima zilizoandaliwa na benki ya NMB Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa uelimishaji kuhusu huduma za bima baada ya benki hiyo kuwa benki wakala wa bima yaani Bancassurance Agent.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema, umefika wakati sasa Wananchi kwa wingi wajiunge na huduma za bima pamoja na matumizi yake ili kujikinga na majanga yanayoweza kujitokeza na hivyo kuathiri masuala ya kiuchumi. Alisisitiza umuhimu wa kuwa na bima zinazotolewa nchini kulingana na hitajio la kila anayehitaji.

“Huduma hii ya Bancassuarnce imeleta msisimko katika soko la bima kwa kiwango kikubwa sana kupitia matawi ya NMB yaliyoko nchini” alisema Mhe. Majaliwa na kueleza kuwa Watanzania hususan walioko vijijini ambako benki imefungua matawi na wakala itaweza kutoa huduma hiyo kwa urahisi”.   Akieleza Zaidi kuwa usambazaji wa huduma ya bima kwa jinsi hii umekuwa chachu kwa  maendeleo ya Watanzania wote.

Mkuu huyo, aliipongeza NMB kwa kutoa huduma stahiki za kifedha kwa njia mbalimbali ili Wananchi wapate kunufaika “nawapongeza NMB kwa kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli hususan katika kutoa huduma za kifedha jumuishi ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa huduma ya bima kupitia mtandao”.

Akitoa salama za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini(TIRA), Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Said alizitaka benki nchini kuchangamkia fursa ya kuwa benki wakala wa bima ili kutoa huduma kwa Wananchi kwa wingi. Alisema “mpaka  sasa  ni benki 13 tu ambazo zimesajiliwa kutoa huduma za bima kwenye benki - Bancassurance, kwa namba hii bado benki hazijatumia fursa hii ipasavyo”.

Aliongeza kuwa “naomba nichukue fursa hii kuwashajihisha benki nyingine kwani fursa hii ina mambo mtambuka ikiwemo kuajiri vijana wetu katika vitengo vya bima vya benki hizo”. Alizitaka benki ambazo hazijachangamkia fursa hii kuja kufanya usajili wa huduma za bima katika ofisi za Mamlaka. Aidha, aliipongeza benki ya NMB kwa kuchangamkia fursa ikiwa ni miongoni mwa benki zinazotoa huduma za bima kwa kufuata sheria na kanuni elekezi.

Bi. Khadija Said aliongeza kuwa, huduma hii pamoja na kupanua wigo wa huduma za bima ambazo zitaongeza pato la Taifa kupitia sekta ndogo ya bima, ikienda sambamba na uwekaji wa mifumo thabiti ya TEHAMA itakayotumika kusimamia huduma hii na kukusanya mapato ya nchi inavyostahiki.

 

Mbio hizo zilizozinduliwa na Waziri mkuu, zilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Uongozi wa benki ya NMB.