Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TUNAJALI AFYA YAKO: TIRA YAKABIDHI OFISI YA WAZIRI MKUU BIMA ZA AFYA 1,093 KWA WENYE MAHITAJI MAALUMU
17 Sep, 2024
TUNAJALI AFYA YAKO: TIRA YAKABIDHI OFISI YA WAZIRI MKUU BIMA ZA AFYA 1,093 KWA WENYE MAHITAJI MAALUMU

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imekabidhi kadi za bima ya afya 1,093 kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa wakati wa Baraza la Maulid leo Septemba 16, 2024 mkoani Geita.

Awali kabla ya kukabidhi kadi hizo Kamishina wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware alisema 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alisaini Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI) namba 13 ya mwaka 2023 ili kuwezesha watanzania wote kunufaika na bima.

Katika kukamilisha azma hiyo, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakar Zuber bin Ally na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware walianzisha zoezi la kutoa bima za afya 10,000 kwa watanzania mbalimbali bila kujali tofauti zao.

Awamu ya kwanza ya utoaji bima hizo elfu kumi, Dkt. Saqware amekabidhi kadi za bima 1,093   ambapo kadi 500 ni za kampuni ya Assemble na zilizobaki 593 ni za Kampuni ya Strategis. Mchakato wa kadi zilizosalia 8,907 utaendelea kutekelezwa kwa awamu chini ya kamati maalum ya Mufti ili kufikia ahadi ya kadi elfu kumi.

Bima hizo zimekidhi vigezo vyote vya kisheria na kati ya bima hizo wanaume watapata kadi 448 na wanawake kadi 605. Aidha, kadi hizo zimeshalipia hivyo, wanufaika wataweza kupata huduma za afya na matibabu mwaka mzima bila kugharamia chochote kwenye Hospital zote nchini ambazo zina mkataba na Kampuni au Skimu ya bima ya afya.

Wazo hili la kuwafikia watanzania wenye uhitaji wa bima za afya lilikuja wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Mufti chenye maudhuhi ya maadili. 

Zoezi hili kwa upande wa pili litawaunganisha watanzania wengi bila kubagua wala kujali dini, kabila, jinsia ama umri kwa kuwa suala la afya ni la watanzania wote.