Makampuni 22 ya Bima nchini Yaungana Kukinga Miradi Mikubwa
Hivi karibuni sekta ya bima nchini imeanzisha bima ya kukinga miradi yenye thamani kubwa bila kutegemea makampuni ya bima ya nje ya nchi kama ilivyokuwa awali.
Makampuni ya bima 22 ya hapa nchini yameungana kwa pamoja ili kutengeneza mfuko mmoja ambao utatumika kukinga majanga mbalimbali kwenye miradi mikubwa. Kwa kuanza umoja huo utakinga vihatarishi kwenye uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi yaani Insurance Consortium for Oil and Gas.
Hafla ya uzinduzi wa Consortium ulifanywa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Chande (Mb) mwishini mwa juma katika Hoteli ya Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam. Mhe. Chande alisema kuwa siku za nyuma, kwa sababu ya ukwasi na mitaji midogo, makampuni ya bima yasingeweza kukinga vihatarishi vya majanga kwa miradi mikubwa kama ya mafuta na gesi na hivyo kufanya makampuni ya kigeni kutoa kinga kwa miradi kama hiyo.
Mhe. Chande alisema muungano huu utasaidia makampuni ya bima kuongeza uwezo wa kuhimili vihatarishi hali ambayo itasaidia pia ubakishaji (retantion) wa fedha za ada za bima nchini kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Alichukua nafasi hiyo kuwataka wanaoshirikiana katika consortium hiyo kuhakikisha wanatumia fursa vizuri kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Kamishna wa Bima nchini alielezea hatua ya kuwa na consortium maalum kwa ajili ya mafuta na gesi ni kuunganisha nguvu za makampuni ya bima ili yaweze kukinga majanga kwa pamoja kwani misuli ya ukwasi na mtaji inakuwa imara zaidi. Alimfahamisha Mhe. Naibu Waziri kuwa kutokana na mapinduzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo yanayofanywa na Serikali inayotuongoza, kwa sasa hitajio la consortium ni kubwa kwa sababu uwekezaji na miradi mikubwa unalazimu uwepo wa consortium na watoa huduma za bima hapa kwetu nchini wameamua kuchukua fursa hiyo.
Aidha, Kamishna wa Bima alisema, mategemeo ya Mamlaka ni kuona mkataba uliosainiwa na makampuni ya bima kwa nia ya umoja huu (consortium) unafanyakazi kulingana na makubaliano katika mkataba huo. Alisisitiza kuwa, TIRA itaendelea kuangali utendaji wake kuhakikisha faida zilizoainishwa zinakuwa na tija kwa Taifa, Wananchi pamoja na wawekezaji nchini.