Bima na bonanza,TIRA inasema; elimu ya bima lazima ianzie ngazi za msingi: klabu za bima za wanafunzi Arusha DC zafana
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Kaskazini imeandaa bonanza maalumu lililowashirikisha wanafunzi kutoka shule 36 ambao ni wanachama wa klabu za Bima kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi kuhusu masuala ya bima .
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha, Afisa bima wa TIRA kanda ya kaskazini, Caroline Makiluli amesema kuwa, wameamua kukutana katika viwanja vya michezo shule ya sekondari Ilboru kwa ajili ya bonanza hilo ambalo limewashirikisha wanafunzi waliopo katika klabu za bima Arusha DC.
Amesema kuwa lengo kubwa la bonanza hilo ni kuhamasisha matumizi ya bima nchini kwani wanafunzi ni Taifa la kesho; hivyo, ni vizuri wakafahamu Mamlaka inavyofanya kazi pamoja na kuwa na uelewa wa bima na bidhaa zake kwa namna gani zinavyoweza kuwanufaisha.
Amesema kuwa bonanza hilo ni fursa muhimu sana kwa wanafunzi na kwa mabalozi wa bima ambao ni walimu wanaofundisha masuala ya bima mashuleni.
Amefafafanua kuwa,bonanza hilo limeshirikisha jumla ya shule 36 zilizopo kwenye Halmashauri ya Arusha DC ambapo wawakilishi kutoka shule hizo ndio wameweza kuhudhuria katika bonanza hilo .
'Hii njia tuliyotumia ya bonanza ni njia nzuri mojawapo kwa kuwa wanafunzi hao wataenda kupeleka taarifa kwa watu mbalimbali kufahamu TIRA na majukumu yake Pamoja na kufahamu kuhusu bima kwani hawa ndio watumiaji wa baadaye wa bidhaa za bima. Aidha wapo ambao wananufaika na bidhaa hizi kwa sasa"amesema Caroline.
Amesema kuwa,malengo ya Mamlaka ni kuwafikia wananchi wengi iwezavyo na hii ni mwanzo tu bado wanaendelea kwa mkoa mzima wa Arusha kwani wanatamani wapate kizazi kinachotumia bidhaa za bima ili kiweze kuendelea mbele kiuchumi.
Amesema kuwa,michezo iliyohusika katika bonanza hilo ni michezo ya kuvuta kamba, chemsha bongo ambapo wameweza kujibu maswali mbalimbali kuhusu bima, mchezo wa draft pamoja na mchezo wa mpira wa miguu na pete.
Amesema kuwa wamefikia hatua ya kutumia njia ya michezo kufikisha ujumbe kwa jamii kwani ndiyo sehemu ambayo makundi mbalimbali wanakutana na ni sehemu ya kuongeza umoja wetu.
Kwa upande wake Mwalimu Upendo Gervas ambaye ni Balozi wa bima kutoka shule ya sekondari Kiserian na Mwenyekiti wa mabalozi wote wa shule za sekondari kwa Arusha DC amesema kuwa kilichowakutanisha kwenye bonanza ni kuitangaza bima kwa watu wote waitambue bima na kuweza kuitangaza katika maeneo mbalimbali .
Amesema kuwa watu wengi wana elimu nodgo kuhusu masuala ya bima na baadhi wanayo elimu ya bima ya Afya. Bima zipo za aina nyingi kwa mfano bima ya moto, bima ya maisha, n.k. Hivyo, wanafunzi wanafunzi wakielewa bima vizuri watakuwa mabalozi wa bima wazuri.
"Mashuleni kuna ratiba kwa ajili ya klabu mbalimbali, wanapewa elimu, wanajiandikisha kila Alhamisi, wanakaa pamoja na kufundishwa kuhusu masuala ya bima na kuna wanafunzi wengine wameshaanza kuweka akiba baada ya kupata elimu hiyo na kutambua kumbe hawajui kesho yao, na wameshajua kuwa wanaweza kuweka bima kuhusu elimu kwani hatujui kesho yetu ili kama wazazi hawapo wasitetereke kwenye masomo yao."amesema.
Kwa upande wao wanafunzi hao Thomas George amesema kuwa elimu waliyoipata kuhusu bima ina faida kubwa sana katika maisha yao na hilo bonanza la bima litahamasisha watu kujua umuhimu wa bima na kuwapa hamasa ya kufahamu matumizi ya bima .
Amesema kuwa, kwa sasa baadhi ya huduma zinahusisha matumizi ya bima na hata kazi nyingi ambazo tunazifanya ni muhimu kuwa na bima kusudi pale utakapopata janga lolote unalipwa fidia ya bima kutokana na janga hilo .
Naye mwanafunzi mwingine amesema kuwa ,elimu hiyo imemsaidia katika kujua umuhimu wa bima kwani umuhimu wake inakufanya upate huduma kiuwepesi, mfano bima ya afya inatoa uhakika wa kupata huduma ya afya kwa urahisi na uwepesi na pasipo kutumia fedha taslimu.
"Bima ni muhimu sana maana unapata huduma kiuwepesi na tunapopitia changamoto yoyote ili kutatua hiyo changamoto lazima uwe na bima kwani ndiyo itaweza kukusaidia kurejeshwa kwenye hali uliyokuwa nayo kabla ya changamoto hiyo. Hivyo ni jambo muhimu sana wananchi wahakikishe wanatumia huduma/bidhaa za bima kwa kiwango kikubwa."amesema.
"Nashauri serikali ianzishe elimu ya bima mashuleni na iwekwe kwenye mitaala kabisa kwani ili watu wajue umuhimu wa bima lazima wafundishwe na kuweza kuifahamu bima."
Naye Mwanafunzi mwingine Glory Mlay amesema kuwa wao kama wanafunzi wamekuwa wakiwashawishi wazazi pamoja na jamii nzima waweze kuwakatia bima kwani tayari wana uelewa mkubwa kuhusu faida na matumizi ya bima .
Amesema kabla ya kupata elimu hiyo hakujua kama ina umuhimu mkubwa kiasi hicho hivyo alivyopata elimu hiyo amejua faida zake na atahamasisha jamii kuweza kukata bima kwa wingi kwani ina manufaa makubwa sana.