‘’BIMA NI KINGA NA UWEKEZAJI’’ - KAMISHNA WA BIMA TANZANIA, DR. BAGHAYO: MAADHIMISHO WIKI YA BIMA 2024
Wiki ya Bima imeanza rasmi leo Septemba 13, 2024 jijini Dodoma. Ambapo Kilele cha Wiki ya Bima nchini kitaadhimishwa hapo kesho Septemba 14, wadau mbalimbali wa Bima wamekusanyika kwa pamoja na kufanya matembezi ya kilometa tano kutoa elimu ya bima nchini na matumizi ya huduma za bima.
Wiki ya Bima imeandaliwa na Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA). Lengo likiwa kuwaleta pamoja wadau wa bima na kujadili mambo mbalimbali kuhusu sekta hiyo muhimu hapa nchini. Na hufanyika kila mwaka.
‘Utaratibu huu (maadhimisho) unasaidia wananchi kuamini sekta ya bima na kutumia huduma mbalimbali za bima ambazo zitawasaidia kuondokana na umaskini. Bima ina dhumuni la kutoa kinga na pia ni uwekezaji hivyo tunawashauri watanzania wote watumie bima” amesema Dr. Baghayo Saqware, Kamishna wa Bima Tanzania.
Pia Mhe. Janet Mayanja Mkuu wa Wilaya ya Chamwino akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amepongeza sekta ya bima nchini na kusisitiza elimu ya bima iendelee kutolewa kwa wananchi ili wazitumie kwa faida yao.