Dkt. Jafo asisitiza miradi ya kimkakati kukatiwa bima na kampuni za Ndani.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amesisitiza kuwa Miradi ya kimkakati inayoendelea nchini ikatiwe bima na kampuni za bima za ndani ya nchi ili kukuza sekta ya bima nchini.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo tarehe 5 Januari 2025 alipotembelea Banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika Maonesho ya 11 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dimani Fumba kuanzia Januari 1 – 15 ambapo leo ni uzinduzi rasmi.
“TIRA kama Mamlaka ili kukuza Sekta ya Bima nchini Tanzania Bara na Visiwani, hakikisheni Miradi yote ya Serikali ya Kimkakati inakatiwa bima na kampuni za bima za ndani ili kubakisha Fedha nchini na hii itasaidia kupanua wigo katika Sekta ya bima” alisema Dkt. Jafo ambaye ndiye Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi huo.
Aidha, Bi. Awanje Matenda Meneja wa Mamlaka Ofisi ya Kanda ya Unguja ambaye amemuwakilisha Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija I. Said alimueleza Mhe. Waziri kuwa TIRA ina Majukumu ya kusajili, kusimamia na kuendeleza soko la bima nchini, na pia kubainisha mikakati inayoendelea katika soko la bima kwa sasa. Alimueleza Mhe. Waziri pia kuhusu majukumu ya Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania.
Mamlaka inashiriki maonesho haya kama muendelezo wa utoaji elimu na uhamasishaji kuhusu matumizi ya bima
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA