Dkt. Saqware atoa wito kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kufichua Udanganyifu katika bima
Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware alitoa wito huo wakati wa Mafunzo maalum kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) yakiwa na lengo la kuimarisha uelewa wa masuala ya bima kwa vyombo vya Habari. Semina hiyo imefanyika leo Novemba 18, 2025 TIRA – Bima House Njedengwa, Dodoma.
Aidha, Dkt. Baghayo Saqware akitoa hotuba ya ufunguzi aliwapongeza Wahariri kwa kazi zao nzuri za kuelimisha jamii na kusisitiza vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu masuala ya bima. Lakini pia alieleza juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Mamlaka kuimarisha sekta ndogo ya bima ikiwemo utoaji elimu kwa umma na matumizi ya mifumo ya kidigitali kurahisisha huduma.
Katika Semina hiyo pia mada mbalimbali zilitolewa zikiwemo Usimamizi wa TIRA katika Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na Masuala ya Udanganyifu katika bima ambapo Kamishna alitoa wito kwa Wahariri na kufatilia kesi mbalimbali za udanganyifu ,“Fichueni Wadanyanyifu katika bima kwa kufatilia kwa karibu kesi mbalimbali zinazoendelea katika Mahakama zetu”
Wahariri pia walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali ambapo yalijibiwa kikamilifu na Maafisa wa Mamlaka sambamba na maoni yao kuchukuliwa kwa utekelezaji. Akizungumza kwa niaba ya Wahariri Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Deodatus Balile aliishukuru Mamlaka kwa kuandaa mafunzo hayo kwakuwa yanawajengea uwezo zaidi na kusisitiza eneo la bima ni pana na ni wajibu wa Wahariri kulisemea zaidi kwa wananchi.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA
