Dkt. Saqware awapongeza Suma JKT kwa kuanzisha kampuni mpya ya Bima ya Maisha: Suma JKT Life Insurance

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Mei 10 2025, iliungana na wadau wengine katika sekta ya bima kushuhudia uzinduzi wa Kampuni ya Bima ya Maisha inayoitwa Suma JKT Life Insurance katika hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa The SuperDome Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo Kamishna wa Bima Tanzania Dkt Baghayo Saqware aliwapongeza kwa kuanzisha kampuni hiyo na kuwakaribisha rasmi katika sekta ya bima.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Jacob J. Mkunda. Lakini pia Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware alishiriki na katika hotuba yake alitoa rai kwa kampuni hiyo kufanya kazi kwa weledi, uaminifu, uadilifu na kuwajali wateja lakini zaidi kuwa wabunifu na kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ambayo inakua kwa asilimia 5% na kuahidi ushirikiano kutoka Mamlaka katika kutekeleza majukumu yao.
Awali pia Bi. Flora Minja, Mwenyekiti wa Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI) katika hotuba yake aliwaahidi ushirikiano na kuwapongeza kwa hatua hiyo muhimu katika sekta ya bima.
Akihitimisha Uzinduzi huo Mgeni Rasmi Jenerali Mkunda katika hotuba yake aliishukuru Mamlaka kwa ushirikiano walioonesha katika kufanikisha usajili wa kampuni hiyo na kuongeza nia ya Jeshi pia ni kuendelea kuchangia katika Uchumi wa nchi kuongeza pato la taifa kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa yani Suma JKT.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA