Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
ELIMU YA BIMA KUPITIA UKAGUZI WA VYOMBO  VYA MOTO GEITA
10 Oct, 2024
ELIMU YA BIMA KUPITIA UKAGUZI WA VYOMBO  VYA MOTO GEITA

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na kampuni za bima kwa siku ya tisa (9) leo imeendelea kutoa elimu ya bima kwa wakazi wa mkoa wa Geita na na maeneo ya jirani, katika Maonesho ya saba (7) ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya bombambili mjini hapo. 

Maafisa wa Mamlaka wakiongozwa na Afisa Sheria Mwandamizi Bw. Aderickson Njunwa kwa kushirikiana na kampuni zilizoshiriki, leo Octoba 10, 2024 imetoa elimu ya bima kwa njia ya ukaguzi wa mabasi ya abiria yanayotoka kituo kikuu cha Geita kuelekea maeneo ya Mwanza, Katoro, Sengerema na maeneo mengine,ambapo asilimia kubwa ya vyombo hivyo vimekatiwa bima. 

Zoezi hilo pia liliendelea katika kituo cha kidogo cha mabasi cha Nyankumbu ambapo abiria waliokuwa katika mabasi walipewa elimu ya bima na vipeperushi vinavyoelezea kuhusu utaratibu wa madai na fidia ya bima. 

Jumla ya mabasi ya abiria  arobaini na tatu (43) yalikaguliwa na zaidi ya abiria 1500 walifikiwa. Kwa sehemu kubwa elimu hiyo imelenga kuwaelimisha madereva, watendaji wao na abiria kuhusu umuhimu wa bima, faida ya bima kwa abiria, umuhimu wa kuwa na tiketi na sifa za tiketi halali, njia za kuhakiki uhalali wa bima na pia umuhimu wa kukata kwa ada halali.

Maonesho hayo yanatarajiwa kufungwa Octoba 13 2024 na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.