IGUNGA WAITIKA WITO WA SERIKALI KUKATA BIMA YA ZAO LA MPUNGA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kupitia ofisi ya Kanda ya Magharibi, Tabora ikiwakilishwa na Meneja wa Kanda hiyo Dkt. Emmanuel Lupilya imetoa elimu ya bima na kuwahamasisha wakulima wa Kijiji Cha Mwampuli, Wilaya Igunga mkoani Tabora katika tukio
muhimu ambapo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Matiko Chacha alikua mgeni rasmi.
Wakulima hao wa zao la Mpunga wamepewa elimu ya bima na kuhamasishwa umuhimu wa kukata bima ya zao hilo kwa kufuatia melekezo ya Serikali yanayomtaka kila mkulima kuwa na bima ya kilimo kwa ajili ya kuwasaidia waweze kusonga mbele zaidi na sio kurudi nyuma pindi wanapopatwa na majanga yasiyotarajiwa.
Mhe. Chacha amesisitiza kwamba Bima ni huduma isiyopingika na ni maelekezo ya Serikali kuwa kila mkulima lazima awe na Bima ya kilimo. Hivyo, ni vema wakulima wakatumia fursa hiyo kuitikia wito huu ili kuhakikisha wanashiriki kwenye kilimo kwa tija.
Dkt. Lupilya akiiwakilisha Mamlaka amesema kuwa kwa sera iliyopo inaelekeza kila mkulima anapaswa kuwa na bima kwa ajili ya maghala ya mpunga, mashine za kilimo cha mpunga mpaka kiwandani, Bima ya Shambani ili kujikinga na majanga yasiyotarajiwa, yanayopelekea kupunguza wastani wa makisio ya mavuno, ubora wa zao la mpunga, lakini kubwa ni kutumia Bima hiyo kwa ajili ya Mkopo kwenye taasisi za fedha.
Aidha, kupitia uhamasishaji uliofanywa na Mamlaka wakulima, viongozi wa bodi, mameneja, katibu meneja, wajumbe wa bodi na viongozi wa AMCOS zaidi ya 500 wameitikia wito wa Serikali kwa kuonyesha utayari wa kuchukua tahadhari ya kujikinga na majanga yasiyotarajiwa kuanzia msimu huu wa kilimo 2024/2025 kwa kukatia bima mazao na maghala yao.