ELIMU YA BIMA KWA KIZAZI KIPYA: WANAFUNZI WA BAOBAB WATEMBELEA TIRA KUJIFUNZA KUHUSU UELEWA WA BIMA
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Baobab, wametembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) leo, Agosti 9, 2024, kwa lengo la kujifunza kuhusu majukumu ya Mamlaka, na umuhimu wa bima kwa ujumla.
Kupitia programu ya mafunzo kwa vitendo, maarufu kama 'Study Tour', wanafunzi hao walipata fursa ya kushiriki katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoendeshwa na wataalamu wa bima akiwemo Bi. Irene Horera, Afisa Ubora, Bw. Ali Khalifan, Afisa Mtakwimu Bima, na Bw. Lusungu Mbilinyi, Afisa Bima.
Wanafunzi hao walipata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ambayo Mamlaka inatekeleza, umuhimu wa kuwa na bima, na fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya bima. Elimu hii waliyoipata inalenga kuwapa uelewa wa kina wa masuala ya bima ili wawe mabalozi bora wa bima kwa wanafunzi wenzao.
TIRA wakati wote inasisitiza elimu ya uelewa wa bima kuanzia kwa vijana wadogo ili kadri wanakuwa watambue umuhimu wa kuwa na bima na faida zake.
Katika juhudi za kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na elimu ya bima, zoezi hili limezingatia mikakati endelevu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) kujenga vizazi vyenye uelewa wa bima ili hatimaye wawe watumiaji wa huduma na bidhaa za bima.