Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji kwa Umma yaridhishwa na Utendaji wa Mamlaka ya Usimamizi Wa Bima Tanzania - TIRA
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji kwa Umma (PIC) imeridhishwa na utendaji wa Mamalaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania- TIRA na kusema kuwa Mamlaka toka kuanzishwa kwake imekua ikiendelea kukua kila mwaka bila kuterereka mbali ya kuwa ni Taasisi ya Serikali inayojiendesha yenyewe kwa asilimiamimoja.
Hayo yameelezwa leo Januari 9, 2025 Bungeni jijini Dodoma na Mkt. wa PIC Mhe. Augustine Vuma Holle- Mbunge waKasulu Vijijini wakati akichangia taarifa ya Utendaji wa TIRA iliyowasilishwa mbele ya PIC. Mhe. Holle ameendelea kusema kuwa taarifa ya utendaji wa TIRA inaonesha wazi kuwa taasisi hiyo imejipanga kutekeleza majukumu yake ipasavyo na hivyo kuwataka TIRA kuendelea kusimamia watoa huduma za bima kwa uthabiti zaidi ili kuendelea kuleta tija kwa wananchi na serikali kwa jumla.
Akitoa taarifa ya utangulizi kwa PIC Mkt. wa Bodi ya Taifa ya Bima CPA. Moremi Marwa amesema kuwa Bodi ya Taifa ya Bima inaendelea kuisimamia Mamlaka ili kuhakikisha kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake kama ilivyokusudiwa na Serikali na kusema kuwa kwa ujumla Bodi inaridhika na kiwango cha utendaji wa TIRA ambao umewezesha kupatikana kwa mafanikio mbalimbali mathalan mchango wa bima kwa taifa umefikia asilimia 2.01 kwa mwaka wa 2023 ikilinganishwa na asilimia 1.99 kwa mwaka 2022. CPA Moremi Marwa amemalizia kwa kusema kuwa mafanikio yote hayo yamechangiwa na mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara na sera nzuri zinazotekelezwa na Serikali na Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Awali Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware, alieleza mbele ya PIC kuwa Kwa mwaka 2023 takwimu zinaonesha kuwa, asilimia 69.6 ya kampuni za bima nchini zinamilikiwa na Watanzania. Hali hi inayoonesha kuwa watanzania wanashiriki
kuwekeza katika Sekta ndogo ya bima hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wanchi. Vilevile Kamishna alieleza kuhusu majukumu ya TIRA, hali ya ukuaji wa sekta, uandikishaji wa ada za bima na malipo ya fidia za bima ambapo maeneo yote hayo yanaonesha ukuaji wa sekta ya bima.
Akihitimisha wasilisho lake Kamishna wa Bima amesema kuwa Mamlaka chini ya usimamizi wa Bodi ya Taifa ya Bima itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye Sekta ya Bima kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia Soko la Bima kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayowekwa na Serikali. Aidha, Mamlaka itaendelea kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha kuwa Soko la Bima nchini linaendelea kuwa salama, endelevu, lenye ushindani na tija kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Nao kwa upande wao Waheshimiwa Wajumbe wa PIC wameitaka TIRA kuendelea kuweka mazingira yenye usawa wa ufanyaji wa biashara baina ya kampuni na watoa huduma wote wa bima nchini.