Kamishna wa Bima afungua mafunzo ya Bima Mtawanyo
Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware leo amefungua mafunzo ya siku mbili kwa wataalamu wa bima mtawanyo kutoka kampuni za bima nchini yanayofanyika katika kumbi za mikutano za hoteli ya Ramada jijini Dar es Salaam.
“Mafunzo ya aina hii ni kipaumbele cha serikali katika sekta ya bima nchini kwani tumelenga kuhakikisha tunakuza uwezo wa wataalamu katika soko la bima hususani katika kuandikisha majanga makubwa” alisema Dkt. Saqware.
Dkt. Saqware amewataka wataalam waliohudhuria katika mafunzo hayo kutumia fursa hii kwa ufasaha ili kuhakikisha soko la bima linakuwa na wataalamu wa kutosha.
“Ni imani yangu kuwa baada ya mafunzo haya mtakuwa na ujuzi na uelewa wa kutosha katika kuandikisha na kuandaa mikataba sahihi ya bima mtawanyo katika maeneo ya Bondi, Bima za Shughuli za Ujenzi na maeneo mengine ambayo yanahitaji wa bima mtawanyo” alisema Dkt. Saqware.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na kuratibiwa na kampuni za bima mtawanyo Tanzania (Tanzania Reinsurance Company) na Kampuni ya Bima Mtawanyo (Fair Reinsurance Brokers) kutoka nchini Morocco yanahusisha watalaamu zaidi ya thelathini kutoka kampuni za bima nchini.
Kamishna amewashukuru waandaji wa mafunzo haya kwani yamekuwa na manufaa kwa soko la bima nchini na yanaendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Moroocco ambao umedhihirishwa katika maeneo na nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.