Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
KAMISHNA WA BIMA AHITIMISHA ZIARA ELIMU YA BIMA KANDA YA KUSINI LEO AGOSTI 15, 2024
15 Aug, 2024
KAMISHNA WA BIMA  AHITIMISHA ZIARA ELIMU YA BIMA KANDA YA KUSINI LEO AGOSTI 15,  2024

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imeendelea kuisimamia vema sekta ya bima nchini kwa kuhakikisha kuwa watumiaji na wanufaika wa huduma za bima wanafikiwa huku watoa huduma za bima wakiendelea kuongezeka na kuchochea kukua kwa soko, maendeleo na ustahimilivu wa sekta ya Bima nchini kwa ujumla.

Hili limedhihirishwa na hatua iliyochukuliwa na  Mamlaka ya Usimamizi wa Bima kufuatia ziara ya Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware akiambatana na ujumbe wake wa viongozi mbalimbali wa Mamlaka wakiwemo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Hawa Mniga, Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na Maendeleo ya Soko, Bw. Samwel Mwiru, Kaimu Meneja Ubora na Udhibiti Vihatarishi, Bw. Pastory Mabonesho na Afisa Uhusiano kwa Umma Mwandamizi, Bw. Abubakari Kafumba.

Ziara hii imeacha mwangwi katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini huku mwitikio wa elimu ya bima ukiwa ni wenye kuridhisha. Zoezi hili lililenga kuifikia mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Mtwara na Lindi ambapo katika awamu hii ya kwanza Mamlaka ilitoa elimu ya bima kuanzia ngazi ya Uongozi wa Mkoa kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala pamoja na watumishi wao ili kuwajengea uwezo na kuwapa elimu kuhusu masuala ya bima ili na wao wawe mstari wa mbele kusambaza elimu ya bima na kuhamasisha matumizi ya huduma na bidhaa za bima kwa wananchi wa maeneo yao.

Akihitimisha ziara hiyo rasmi leo Agosti 15, 2024 katika Mkoa wa Lindi Dkt. Saqware amesema Mamlaka imeendelea kuisimamia vema sekta ya bima nchini ikiendelea kukua kwa asilimia 15 kila mwaka na kuchangia katika pato la taifa kwa asilimia 2. 

Kupitia zoezi hili la uelimishaji Dkt. Saqware ameeleza kuwa bima inatoa kinga ya mali, afya na uwekezaji. Amesema,”Elimu hii tuliyotoa tuitumie kama fursa ya kuwekeza katika sekta ya bima na tuwashawishi pia watanzania wengine watumie bima. Matarajio yetu ni kuona kila mtanzania anashiriki kwenye sekta ya bima”.

Aidha, kwa upande wa bima ya afya, Kamishna wa Bima amebainisha kwamba Serikali imeshapitisha sheria ya bima ya afya kwa wote, na kwa mujibu wa sheria hiyo kila mmoja atapaswa kuwa na bima ya afya.

Kupitia vikao vilivyofanyika katika ngazi ya mkoa kupitia ziara hiyo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima imewaomba wakuu wa mikoa yafuatayo: Wakuu wa Mikoa kuwahamasisha wakuu wa wilaya, Makatibu tawala na wananchi wa mkoa husika kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote, Mamlaka kushirikiana na ofisi Mkuu wa Mkoa katika kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi wa mkoa husika kwa lengo la kujenga uelewa wa bima ili wabaini manufaa ya kutumia bima kama kinga mahsusi kwa maisha, afya na mali zao; na pia kuwaomba Wakuu wa Mikoa wawe Balozi wa TIRA katika utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi wanaowasimamia, kuwahamasisha kutumia bidhaa na huduma za bima, hususan bima za afya na kilimo.

Kwa mantiki hii, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imeendelea kusimamia sekta ndogo ya bima kwa tija na ufanisi na hivyo kuifanya sekta hiyo kuendelea kutoa kinga za bima stahiki kwa mali, maisha na afya za watanzania.
 
Aidha, Mamlaka inaendelea kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini; Mkakati wa Taifa wa utoaji Elimu ya Bima kwa Umma; na Mkakati wa Kitaifa wa Huduma za Bima Jumuishi.
 
Mamlaka itaendelea kuhakikisha soko la bima la Tanzania linaendela kuwa himilivu, lisilo na udanganyifu, lenye weledi na lenye tija.