Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Kamishna wa Bima Tanzania aeleza viashiria kupima utendaji Soko la bima  
23 Nov, 2024
Kamishna wa Bima Tanzania aeleza viashiria kupima utendaji Soko la bima  

Uzinduzi wa Taarifa ya  Utendaji wa  Soko la Bima kwa mwaka 2023 umefanyika hapo jana Novemba 22, 2024 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa SuperDome, Masaki.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ndio waandaji wa tukio hilo ambapo taarifa hiyo imeangazia viashiria mbalimbali vinavyoonyesha ukuaji chanya wa soko la bima hapa nchini. Mgeni Rasmi akiwa ni Naibu Waziri wa fedha Mhe. Hamad H. Chande. 

Kamishna wa Bima Tanzania Dr. Baghayo Saqware akitoa hotuba yake ameeleza viashiria hivyo ni pamoja na ongezeko la watoa huduma za bima, Idadi ya wakata bima,

Ongezeko la uandikishwaji  wa ada za bima, ulipaji wa madai, wastani wa matumizi ya fedha katika bima kwa mwananchi mmoja mmoja, michango ya bima katika pato la taifa, thamani ya mitaji lakini pia ubakizaji wa ada za bima nchini. 

Dr. Saqware pia alieleza njia ya mafanikio katika sekta hii ni kuendelea kuwa na ongezeko la asilimia 15% kwa mwaka  la watanzania wanaotumia bima ili kufikia lengo la asilimia 50% la ongezeko la watanzania wanaotumia huduma za bima ifikapo mwaka 2050. 

Lakini pia njia nyingine ni kuongezeka kwa uwekezaji endelevu, ushirikiano na wadau na matumizi ya teknolojia.

Hafla hiyo pia ilikuwa na mjadala mahsusi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote ulioshirikisha wadau mbalimbali wa taasisi za serikali na binafsi ambao ulichanganua mkakati wa kufanikisha na unafuu wa matibabu utakaopatikana kwa watanzania. 

#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA