Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
KAMISHNA WA BIMA TANZANIA ASIKILIZA MAONI NA KUTOA UFAFANUZI MASUALA YA BIMA AKUTANA NA KAMPUNI ZA BIMA ZANZIBAR
31 Aug, 2024
KAMISHNA WA BIMA TANZANIA ASIKILIZA MAONI NA KUTOA UFAFANUZI MASUALA YA BIMA AKUTANA NA KAMPUNI ZA BIMA ZANZIBAR

Kamishna wa Bima Tanzania, Dr. Baghayo Saqware leo jumamosi, Agosti 31 amekutana na wadau wa kampuni za Bima Zanzibar katika ofisi za Mamlaka visiwani humo kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu bima. 

Wawakilishi wa kampuni hizo za bima walitoa maoni na changamoto zao mbalimbali ambazo zilisikilizwa na kutolewa ufafanuzi na Kamishna wa Bima Tanzania pamoja na Naibu Kamishna wa Bima Tanzania Bi. Khadija Said. 

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na mameneja wa TIRA Zanzibar kwa upande wa ofisi ya Unguja na Pemba. 

Dr. Saqware amezitaka kampuni hizo za bima kuendelea kuweka mikakati mbalimbali katika utoaji wa elimu ya bima ili kila mtanzania aweze kufahamu umuhimu wa bima na kunufaika na huduma hiyo, pia moja ya changamoto iliyotajwa na wadau hao ni udanganyifu katika bima ambapo Kamishna wa Bima Tanzania amesema,

“Udanganyifu katika bima ni jambo ninalotamani kuona limeisha, tunaendelea kulifanyia kazi na ikiwa kuna mashaka yoyote juu ya udanganyifu ni vizuri mtutaarifu mapema’’. 

Pia Naibu Kamishna wa Bima Tanzania amesisitiza kampuni hizo za bima kuendeleza ushirikiano wa pamoja na akizisisitiza ziendelee kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa umma. 

Kikao hicho kimeenda sambamba na kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Bima Zanzibar yaliyofanyika katika uwanja wa Mao Zedong leo Agosti 31, 2024, mgeni Rasmi akiwa ni Mhandisi Zena Said Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar.